WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, leo amezindua rasmi Baraza la Taifa la kutokomeza malaria nchini ambalo lina wajumbe 19.
Baraza hilo lina lengo la kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali ili kuziba pengo la kutengeneza afua ya udhibiti malaria ili kufikia lengo la kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030.
Baraza hilo linaongozwa na Mwenyikiti wake Leodegar Tenga na wajumbe ni Ummy Mwalimu, Mwigulu Nchemba , Nape Nnauye,Dk Wilson Mahela, Dk Jimmy Yonazi, Dk Hassan Abass , Angelina Ngalula,Theobald Thabi, Saimon Shayo.
Wengine ni Mfanyabishara maarufa Said Salim Bakharesa,Mwenyekiti Jumuiya ya Kikristo Tanzania Dk Fredrick Shoo,Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi, Askofu Mkuu Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) Gervas Nyaisonga , Diyan Kimaro, Dk Elen Senkoro.
Wajumbe wengine ni msanii wa kizazi kipya Nassib Abdul ‘Diamond’, msanii Zena Yusuph ‘Shilole’ na Faraja Nyalandu.
Akizugumza katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Malaria leo Aprili 25 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam ,Waziri Mkuu ameelekeza baraza hilo kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali katika sekta zao katika kuchangia juhudi za serikali kupitia sekta ya afya.
Amesema baraza hilo lililoundwa kimkakati linatarajai kufanya kazi kwa mujibu wa ubora wa watu wake katika eneo hilo na hamasa itaanza mara baada ya kuanza kazi hiyo.
“Baraza hili limesheheni watu kutoka sekta michezo, sanaa,utaalamu mbalimbali, ubunifu kwa hiyo tutumie vipaji tulivyonavyo ambavyo Rais ameviona ili kufanikiwa na baada ya uzinduzi itahusisha ukusanyaji wa rasilimali kutoka vyanzo mbalimbali vya ndani ni muhimu zikatekeleza afua muhimu,”alisisitiza.