Baraza la madiwani waikataa rasimu matumizi ya ardhi

MADIWANI wa Baraza la Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro Mkoa wa Arusha wameikataa rasimu ya mpango wa matumizi ya ardhi ya wilaya hiyo, wakidai si shirikishi na inalenga kumega ardhi yao ya malisho na  kuiingiza kwenye hifadhi kitendo ambacho kitaathiri ustawi wa wananchi .

Madiwani hao walitoa kauli hiyo katika baraza hilo baada ya kuwasilishwa kwa ajenda namba nne katika kikao hicho iliyolenga kujadili na kupitisha mpango wa matumizi ya ardhi wa miaka 20 kuanzia mwaka huu 2023 hadi 2043.

Diwani wa kata ya Nainokanoka,Edward Maula alisema hawakubaliani na rasimu hiyo kwa kuwa imelenga kuchukua sehemu kubwa ya ardhi yao na kuifanya sehemu ya eneo la hifadhi jambo litakaloathiri ustawi wa maisha yao na malisho ya mifugo.

Alifafanua kwamba awali serikali ilishachukua asilimia 75 ya ardhi yao na kuifanya eneo la hifadhi ya wanyama pori na misitu na wananchi  kubakiwa na asilimia 25 pekee.

“Sisi kama madiwani tumeweka saini zetu kwa pamoja kukataa rasimu hiyo na sababu za kukataa ni pamoja na serikali kuchukua eneo letu kubwa na kubakiwa na asilimia 25 tu”alisema

Aliongeza kuwa mpango wa matumizi ya ardhi wa wilaya ya Ngorongoro haukufuata matakwa ya sheria ya kushirikisha mikutano  mikuu halali ya vijiji ,hivyo kupitisha mpango huo ni kuhalalisha mwisho wa kuishi kwa kuendelea kukosa makazi,kilimo na nyanda za malisho.

Diwani wa viti maalumu kata ya Kakesio, Tarafa ya Ngorongoro ,Sein Lekeni alisema sababu ya kukataa rasimu hiyo ni kutoshirikishwa kwa wananchi na kupewa elimu juu ya umuhimu wa jambo hilo na iwapo tutaikubali tutakuwa watu wa ajabu sana .

“Leo tulikuwa kwenye kikao cha baraza la madiwani , tumekataa ile rasimu iliyokuwa imeletwa kwenye baraza kwa sababu sio shirikishi ni rasimu ambayo imepangwa na watu fulani ,na tukipitisha tutakuwa madiwani wa ajabu sana ,sisi sote madiwani 32 tumeikataa kwa kuweka saini  zetu ”

Diwani mwingine ,James Moringe wa kata ya Laitore, alisema ajenda ya matumizi ya ardhi ya miaka 20 katika wilaya ya Ngorongoro haina tija na wameikataa kwa sababu imetenga wilaya hiyo kijiografia .

Alisema utaratibu kama huo uliwahi kutumiwa na serikali kupima eneo lao la malisho lenye ukubwa wa kilometa za mraba 1500 na kulifanya pori tengefu  kinyume cha sheria ,suala waliosisitiza kuwa hawakubaliani na rasimu hiyo.

“Hakuna mikutano ya wananchi iliyotumika kuzungumzia suala hilo kuanzia tarafa ya Ngorongoro ambako ndio yaliko makazi ya wamasai”

“Sisi Madiwani wa Wilaya ya Ngorongoro ambao tumeweka saini zetu mpango huu haujawahi kuwa kipaumbele cha halmashauri yetu bali umeletwa na mashirika ya NCAA,FZS na KFW kwenda kuhalalisha uporaji wa Ardhi”

Mwenyekiti wa baraza hilo alisema kuwa rasimu hiyo haikuweza kupita kwa sababu iliandikwa kwa Lugha ya Kiingereza  na madiwani wa jamii ya wafugaji wengi wao hawajui kiingereza hivyo niliamuru ikafanyiwe marekebisho.

“Hii rasimu haikukataliwa ila hiyo rasimu ilikuwa imeandikwa kwa lugha ya kiingereza  na madiwani wengi hawajui lugha ya kiingereza ndio maana niliamuru ikafanyiwe marekebisho ili irudishwe upya katika baraza hilo”

Hata hivyo mwenyekiti huyo alisema anakubaliana na raimu hiyo ila alisema lazima ifanyiwe marekebisho kwani hakuna serikali inayochukia wananchi wake na anaimani mpango wa serikali ni mzuri .

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x