DAR ES SALAAM: BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA), limetoa rai kwa wasanii zaidi ya 1000 wanaofanya shughuli za sanaa kinyume na utaratibu kufanya usajili na kuhuisha vibali vyao ndani ya siku saba kinyume na hapo majina yao yatawekwa hadharani.
Hayo yameelezwa leo na Katibu Mtendaji wa BASATA, Dk Kedmon Mapana ambapo amefafanua kuwa siku zinaanza kuhesabiwa kuanzia leo Mei 06, 2024 ukiwajumuisha wanamuziki wa bongo fleva, singeli, injili, taarab, regae, dansi, hip hop, Dj, mapromota, watozi ‘producers’, wanenguaji ‘dancers’, waigizaji wa video za miziki ‘video vixen’, wazalishaji video za muziki, mameneja, washerehesaji ‘Mc’s’ na taasisi zinazofanya shughuli za sanaa.
“Kuhamasisha wasanii kujisajili barazani ili kufanikisha utambuzi wa wasanii baraza na serikali ili kuwezesha zaidi kwenye sekta ya sanaa katika utendaji kazi wake,
“Ni muhimu wasanii na wadau mbalimbali wawe wanafanya kazi za sanaa ramsi yaani kurasimishwa ambapo katika tafiti inaonyesha zaidi ya wasanii na wadau wa sanaa zaidi ya 1000 wanaendelea kufanya kazi zao bila kuwa na vibali halali,” amefafanua katibu huyo.
Rejea: https://habarileo.co.tz/wasanii-zaidi-ya-6000-kufungiwa/
Mbali na hilo, Mapana amewataka wasanii wote na wadau wa sanaa ambao hawajarasimishwa wafike ofisi za basata kwa ajili ya usajili huku akiwapongeza Alikiba, Zuchu na Diamond kwamba ni miongoni mwa wasanii wakubwa wanaozingatia kanuni na sheria za usajili.