Basata yatakiwa kutafuta vipaji

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pinda Chana amelitaka Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) kuandaa mwongozo wa kutekeleza programu ya sanaa mtaa kwa mtaa ili kuibua vipaji vingi kuanzia ngazi ya chini.

Waziri Chana amesema hayo leo Februari 21, 2023 alipotembelea baraza hilo na kusisitiza kuendeleza ukuaji wa pato la tafa.

“Natoa rai kwenu Basata kuwa na takwimu sahihi kuhusu idadi ya wasanii katika aina zote za sanaa ambazo zitakuwa zinahuishwa kila baada ya muda mfupi na zitasaidia katika upatikanaji wa mikopo pamoja na udhamini kutoka taasisi mbalimbali.” amesisitiza Chana.

Amesisitiza baraza hilo kuendelea kutoa elimu kwa wadau wa sanaa katika kuelimisha na kuburidisha bila kuvunja maadili ya kitanzania.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Pauline Gekul amelitaka baraza hilo kutoa kipaumbele katika sanaa nyingine kama linavyofanya katika muziki pamoja na kutoa fursa kwa vikundi mbalimbali vya maeneo tofauti kushiriki matamasha ya kimataifa.

Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Dk Kedmon Mapana amesema baraza hilo limefanikiwa kuanzisha mfumo wa usajili wa Wasanii Kidijitali, pamoja na kurejesha Tuzo za Muziki.

Habari Zifananazo

Back to top button