WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe ameagiza kukamatwa kwa mmiliki wa Kampuni ya Candia Fresh pamoja na kuifunga kampuni hiyo, kwa kile alichoeleza kuwa inanunua parachichi ambazo hazijakomaa.
Bashe amesema kuwa kampuni hiyo imekuwa ikinunua parachichi hizo changa na kisha kuzitupa katika dampo la Halmashauri ya Mji wa Njombe.
Ametoa agizo hilo leo Jumanne Januari 17, 2022 katika ziara yake mkoani Njombe na kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio lililoonekana kupitia video.
Pia amepiga marufuku wafanyabiashara kuchuma parachichi zikiwa change, kwani hakuna soko linalopokea parachichi ambazo hazijakomaa.
“Wewe (mmiliki wa kampuni) ndiyo ulinunua parachichi kwa nini ulifanya hivyo? Wakati unakwenda kununua ulikuwa na mkataba? Usiondoke kwenye huu msafara askari wako wapi? unaondoka na mimi, ” alisema Bashe.
Amesema maafisa kilimo na watendaji wanatakiwa kuhakikisha wanapita kwenye mashamba na kuzuia utamaduni wa wakulima kuvuna parachichi ambazo hazijakomaa.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Kissa Kasongwa amesema kwa watu wote ambao walivuna parachichi changa walikamatwa kwa makosa mawili ya kukwepa ushuru na kununua maparachichi bila ya kibali.