Bashe: Mradi wa BBT utatengeneza mabilionea

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe amesema mradi wa mashamba makubwa kuwezesha vijana kulima kibiashara (BBT) utatengeneza mabilionea na itakapofika mwaka 2030 atamwonesha Rais Samia Suluhu Hassan mabilionea hao.

Bashe amesema hayo Chinangali II mkoani Dodoma jana wakati wa uzinduzi wa mashamba hayo na akasema vijana waliosajiliwa kwenye programu hiyo watapatiwa mafunzo kwa miezi minne na baada ya hapo watakabidhiwa ardhi yenye hati ya umiliki kwa miaka 66.

Alisema ifikapo mwisho wa mwaka huu au mwezi Juni mwakani, watakuwa na mashamba makubwa ya mbegu yatakayofungwa teknolojia ya kisasa.

“Mashamba haya makubwa tunayoyaanzisha tumeingiza kipengele cha mifugo ili mkulima huyu kijana awe na uhakika wa mbolea, tunaenda kutengeneza mabilionea, tukifika mwaka 2030 wakati tunakusindikiza kwenda kupumzika baada ya kustaafu, Mheshimiwa Rais niulize wale mabilionea wa kilimo wako wapi, nitakuletea mabilionea hao,” alisema Bashe.

Aliwaasa vijana watakaopewa ardhi kwa mara ya kwanza watambue kuwa kilimo si mchezo wa kubashiri na kinahitaji muda kupata mafanikio.

Habari Zifananazo

Back to top button