Bashungwa aja na vipaumbele 9 ujenzi

DODOMA; WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewasilisha bajaeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2024/2025 yenye vipaumbele tisa.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara yake kwa mwaka wa fedha 2024/25 bungeni mjini Dodoma leo, Waziri Bashungwa amesema Wizara ya Ujenzi inatarajia kutekeleza Mpango na Bajeti kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020.

Pia bajeti hiyo itazingatia Mpango Mkakati wa Wizara (2021/22 – 2025/26); Ahadi za Viongozi Wakuu wa Serikali; Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Amesema makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 kwa kuzingatia vipaumbele mbalimbali na kutaja kuwa ni: ” Kufanya matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja iliyoharibiwa na mvua za El Nino na Kimbunga Hidaya.

“Kuendelea na utekelezaji wa miradi inayoendelea. Kuendelea na matengenezo ya barabara na madaraja kwa kutumia makandarasi wa ndani kwa asilimia 100 pamoja na kuhakikisha kuwa barabara zinapitika katika majira yote ya mwaka,” amesema Waziri Bashungwa.

Ametaja vipaumbele vingine ni kuendelea kukijengea uwezo Kitengo cha Ushauri Elekezi wa Miradi cha TANROADS (TECU), ili kiendelee kusimamia miradi mikubwa ya kimkakati;

“Kufanya mapitio ya Sera ya Ujenzi (2003) na Sera ya Taifa ya Usalama Barabarani (2009) pamoja na kanuni na miongozo mbalimbali inayohusiana na sekta ya ujenzi ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na tabianchi;

“Kuendelea kuwajengea uwezo wataalam wa ndani kupitia programu mbalimbali kwa lengo la kuongeza wataalam wabobezi wa ndani ili waweze kusimamia miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa nchini (Local content), Kuendelea kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika utendaji kazi;

“Kutumia teknolojia za gharama nafuu katika ujenzi wa barabara hususan katika maeneo korofi. Kutekeleza Mkakati wa Uimarishaji wa Utendaji kazi wa TEMESA (TEMESA Transformation Strategy 2024 – 2034),” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button