WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa amesema serikali inavutia uwekezaji kwenye sekta ya ulinzi ili kutimiza dira ya Rais Samia Suluhu Hassan kuimarisha sekta hiyo.
Bashungwa aliyasema hayo mjini Kibaha alipokuwa akikabidhi magari matatu ya uokoaji kwa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji yaliyounganishwa na Shirika la TATC Nyumbu Kibaha.
Alisema kuwa wao wanasimamia majukumu yao kikamilifu ili kutekeleza maono ya Rais Samia ya majeshi kushirikiana na wadau wengine kwenye sekta ya viwanda ya ulinzi ili kuvutia uwekezaji kwenye sekta hiyo.
“Magari haya yanaonesha uthubutu wa kutengeneza kitu na uwezo wa majeshi ya Tanzania ambapo kampuni ya Scania ilishangaa kuona ubora huu na kusema haiwezekani Tanzania iagize magari kama haya toka nje kwani uwezo wanao kutengeneza hapa hapa,” alisema Bashungwa.
Alisema vyombo vya ulinzi vinafanyakazi kwa ushirikiano na magari kama haya isiwe kwa ajili ya vyombo vya ulinzi peke yake hapa nchini bali hata na kwa majirani na kwa miaka ya mbele ndoto ni kuuza nchi za jirani.
“Utoaji huduma bora kwenye sekta ya ulinzi unatokana na jinsi Rais Samia alivyoboresha sekta hiyo ili iweze kuhudumia wananchi bila ya kuchelewa hivyo serikali inavutia uwekezaji ikiwemo wa viwanda kwenye sekta ya ulinzi ili dira ya Rais Samia ifikiwe,” alisema.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini alisema kuwa magari hayo yanaonesha jinsi gani nchi ina uwezo wa kuonesha ubunifu wao kwenye teknolojia na wameridhishwa na ubora wa magari hayo.
Sagini alikitaka kikosi hicho kuhakikisha wanafanya matengenezo ya magari hayo kwa wakati ili yadumu kwa muda mrefu kwani magari yanaharibika haraka endapo matengenezo yanachelewa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Nyumbu, Brigedia Jenerali Hashim Komba alisema kuwa shirika lao lilisaini makubaliano na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuunda magari mapya matatu ya kiwango cha Manispaa kwa kutumia Rolling Chassis ya Scania kulingana na hitaji la mteja wao na magari hayo yamekamilika sambamba na utoaji wa mafunzo kwa watumiaji.
Komba alisema kuwa hiyo ni awamu ya pili ambapo ya kwanza shirika lilisaini makubaliano na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kukarabati magari mabovu 12 ya kiwango cha manispaa na magari hayo yalikabidhiwa kwa jeshi hilo baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa ambapo ukarabati wa magari hayo uliokoa gharama kubwa kwani yote haikufikia hata bei ya gari moja jipya la zimamoto.