Bashungwa amsimamisha kazi Meneja Tanroads Lindi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa akitoa maelezo kwa umma kuhusu maandalizi ya kuwapokea Wanafunzi wa kidato cha kwanza mwakani 2023.

LINDI: WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemsimamisha kazi Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi, Mhandisi Andrea Kasamwa kwa kushindwa kusimamia urejeshwaji wa miundombinu ya barabara na madaraja katika Wilaya ya Liwale mkoani Lindi na kusababisha barabara kuu zinanounganisha wilaya hiyo na maeneo mengine kufungwa.

Pia Waziri Bashungwa akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Deo Ndejembi ameshuhudia urejeshwaji wa barabara ya Liwale – Nangurukuru iliyosombwa na maji ikisimamiwa na mtaalam mwenye taaluma ya Falsafa kwa kusaidiwa na wananchi wakati mkandarasi akiwa hayupo eneo la kazi.

Waziri Bashungwa amechukua hatua hiyo leo Machi 6, 2024 wakati akikagua mindombinu ya barabara katika Wilaya ya Liwale na kutoridhishwa na usimamizi wa kazi inayofanywa na Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Lindi.

Advertisement

“Haiwezekani sisi tutoke Dodoma hadi huku Liwale kutokana na changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara iliyopo, Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan amelazimika kutoa helikopta yake tufike huku, lakini hapa site hakuna Mkandarasi, mnaweka mtu aliyesoma falsafa kusimamia kazi ya ujenzi wa barabara,” amesema Bashungwa.

Amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, kupeleka wataalam na kuhakikisha ndani ya siku nne barabara zote kuu na madaraja yanayounganisha Wilaya ya Liwale na maeneo mengine katika mkoa huo ambayo hayapitiki yawe yamefunguliwa na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.