KAGERA: Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ametoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa kagera kurudisha umoja uliokuwepo miaka ya nyuma huku akikemea ubinafsi wa baadhi ya viongozi .
Bashungwa alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya chakula cha jioni ya “Ijuka Omuka sote tuguswe” iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa Kagera, Fatma Mwassa iliyolenga kuwakutanisha wanakagera wanaoishi ndani na nje ya nchi kama sehemu ya kujadili maendeleo mkoani hapo.
“Nakushukuru Mkuu wa mkoa kwa kuandaa jukwaa hili la kujikosoa na kujisahihisha, Rais Dk Samia Suluhu Hassan alipokuwa Mkoa wa Kagera alituelekeza kufanya hili tunalolifanya leo la kujadili mustakabali wa mkoa wetu ili tuone tunawezaje kurudi katika hadhi yetu” amesema Bashungwa.
Amesema kuwa maendeleo ya Kagera yamekuwa yakirudishwa nyuma na baadhi ya viongozi na wanasiasa ambao wamekuwa wakipambania maslahi yao binafsi na kukwamisha maendeleo ya mkoa ambapo kundi moja limejikita katika kuleta maendeleo na kundi jingine limejikita katika kukwamisha maendeleo na kuyapinga .
Aidha, Bashungwa amesema kuwa pamoja na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kutoa fedha za kutekeleza miradi katika Mkoa wa Kagera kama ujenzi wa barabara ya njia nne, stendi ya kisasa na upanuzi wa bandari, bado kumekuwepo na viongozi wanaoendelea kukwamisha utekelezaji huo.
Pia alieleza baadhi ya matukio yaliyochangia kudumaza maendeleo ya mkoa kiuchumi, kijamii na kisiasa ni pamoja na vita, milipuko ya magojwa, majanga ya asili kama tetemeko pamoja na mabadiliko ya tabianchi.
Mkuu wa Mkoa Kagera, Fatma Mwassa amesema mkoa huo hauwezi kuendelea bila ushirikiano kwa kupingana kwa kila jambo, kuwekeana figisu na mikingamo bali mkoa utafanikiwa kwa kuwa na umoja madhubuti.
Amewataka wakazi wa Kagera kuutangaza vizuri mkoa huo na kuusemea mambo mazuri kwa sababu hakuna mtu atataka kuja kuwekeza katika mkoa ambao haujatangazwa kwa mazuri yake.
Comments are closed.