Bashungwa awapa somo wahitimu mafunzo ya ulinzi

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Innocent Bashungwa amewataka wahitimu 65 wa kozi ya stashahada ya kawaida ya masomo ya ulinzi na usalama sanjari na shahada ya uzamili ya sanaa katika masomo ya ulinzi na usalama, kuwawezesha kufikiria na kuchambua matatizo ya usalama, katika mtazamo wa kijeshi.
Bashungwa ameyasema hayo wakati wa kutunuku maofisa hao wa kozi ya 37 ya mwaka 2022/23 kwa maofisa wanafunzi 65 kutoka Chuo Cha Ukamanda na Unadhimu (CSC)kilichopo Duluti Wilayani Arumeru, mkoani Arusha.
Amesema mafunzo hayo yamewashirikisha wahitimu Watanzania 46, pamoja na maofisa wanafunzi 19 kutoka nchi marafiki na kuongeza kuwa maarifa waliyopata kupitia mafunzo hayo yatawawezesha kufikiria na kuchambua matatizo ya usalama, katika mtazamo wa kijeshi.
“Hayati Julius Kambarage Nyerere, muasisi wa taifa letu la Tanzania aliwahi kusema kuwa, ‘bila Umoja, hakuna mustakabali wa Afrika’,sambamba na maneno hayo ya hekima kutoka kwa Mwalimu Nyerere, Tanzania ina uhusiano mzuri sana na wa kirafiki na nchi nyingine,” amesema.
Pia amewapongeza wahitimu wanawake waliohitimu mafunzo hayo na kuongeza kuwa uwepo wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Rais ni hatua muhimu kwa Tanzania kuelekea usawa wa kijinsia.
Amesema uongozi wake makini unatuma ujumbe mzito kuhusu uwezo wa uongozi wa wanawake, na umuhimu wa kuwapa wanawake fursa sawa kwa maendeleo ya mataifa.
Awali Mkuu wa chuo cha Ukamanda na Unadhimu(CSC) Brigedia Jenerali,Sylivester Ghuliku alisisitiza kuwa chuo hicho kitaendelea kushirikiana na nchi mbalimbali kwa ajili ya utoaji mafunzo ya kijeshi na kiutawala.
Wahitimu wengine wanatoka nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Misri, Kenya, Eswatini, Malawi, Msumbiji,Nigeria, Rwanda,Afrika Kusini na Uganda.