WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameipongeza timu ya wataalam kutoka Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), kwa kufanya kazi kuhakikisha wanarejesha mawasiliano ya barabara ya Liwale – Nangurukuru ambayo imeanza kupitika.
Bashungwa ametoa pongezi hizo leo Machi 08, 2024 mkoani Lindi wakati akikagua urejeshwaji wa miundombinu ya barabara na madaraja kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha barabara kuu na madaraja yanayounganisha Wilaya ya Liwale na maeneo mengine kufungwa.
Aidha, Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Mohamed Besta kuweka wakandarasi watatu kwa wakati mmoja kufanya ukarabati upya barabara ya Nangurukuru – Liwale yenye urefu wa kilometa 230.
“Sasa hivi tumefungua barabara ya Nangurukuru – Liwale, maelekezo yangu kwa TANROADS ni kuweka Makandarasi watatu kila mmoja na kipande chake kukarabati upya barabara hii na kuhakikisha barabara inapitika vizuri, hicho ndicho kipimo ninachowaachia Wahandisi na Makandarasi,” amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ametoa wito kwa Makandarasi nchi nzima kuzingatia taratibu na sheria za taaluma ya ukandarasi na kuondokana na hali ya kufanya kazi kwa mazoea na amewataka kuwa wazalendo na kutanguliza masilahi ya nchi wakati wakitekeleza Majukumu yao.
“Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB) na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) ninataka msimamie taaluma hizi, hata TANROADS mnaposaini mikataba simamieni vigezo na masharti yaliyopo kwenye mikataba na kuhakikisha wanaopewa kazi hizo wanakuwa na taaluma na kazi,” amesema Bashungwa.
Bashungwa amewahakikishia wananchi wa wilaya Liwale na Mkoa wa Lindi kwa ujumla kuwa serikali itaendelea kufanya kila jitihada za kuhakikisha hali ya miundombinu na huduma nyingine muhimu zinarejea na kuendelea kutolewa.
Vile vile, Bashungwa ametumia fursa hiyo kutuma salamu za heri Siku ya Wanawake Duniani kwa Rais Samia Suluhu Hassan na wanawake wote nchini.