Bashungwa: JKT italeta mageuzi sekta ya Kilimo

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Innocent Bashungwa amesema JKT haitakuwa kikwazo cha  maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuleta mageuzi ya kilimo hapa nchini.
Bashungwa ameyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa kilimo wa SumaJKT Mngeta Platation.
Aidha, Bashungwa alisema mkakati wa Wizara yake ni kuweka kipaumbele JKT katika bajeti ya mwaka 2023/24 ili waweze kuzalisha maradufu na kwa tija.
“Kwa sasa tuko kwenye mchakato wa maandalizi ya bajeti na kipaumble cha Wizara ni SumaJKT Mngeta Platation ili kuwezesha JKT kufanya mara dufu ya haya wanayoyafanya sasa na kitakuwa ni kipaumbele cha kwanza cha wizara.”Alisema
Alisema kutokana na maono na maelekezo ya Rais na Amiri Jeshi Mkuu ndiyo yaliyofanya mashamba hayo yasimame na  kuwa na mafanikio makubwa.
“Kwa muda mrefu mashamba haya yalikaa bila matumizi yoyote baada ya mwekezaji kushindwa kuyaendeleza, namshukuru Rais na Amiri Jeshi Mkuu na ni maono yake kwa kutambua vijana wengi hawana ajira akaelekeza mashamba haya yawe chini ya Jeshi la Kujenga Taifa.

”Amesema

Oktoba 2021 Serikali ilifikia uamuzi mradi huo wa Mngeta Plantation ambao huko Halmashauri ya Mlimba wilayani Kilombero mkoani Morogoro iwe chini ya taasisi ya SumaJKT na tayari imeshaanza uzalishaji wa mbegu ya mpunga na mahindi.
“Kutokana na nidhamu na ubunifu wa jeshi iliyonayo mmeona ubunifu umezaa matunda tayari hapa JKT inazalisha mbegu kwa ajili ya wakulima wetu.”Amesisitiza
Alisema baada ya Rais Samia kuridhia SumaJKT kukabidhiwa mashamba hayo JKT imeanza kutoa mchango mkubwa kwenye uzalishaji na upatikanaji mbengu za mpunga na mahindi.
Alisema pia hatua ni katika kutekeleza mkakati wa Serikali wa kuwa na usalama wa chakula wa nchini na wananchi na ziada kuuza nje na kusisitiza kuwa JKT iko kwenye mwelekeo mzuri.

“Nikupongeza Mkuu wa JKT (Meja Jenerali Rajab Mabele) kwa usimamizi mzuri wa mashamba haya ya SumaJKT Mngeta Plantation.
“Kimkakati JKT kuwepo mahali hapa pia inasaidia katika masuala ya ulinzi wa vyanzo vya maji ambayo yanakwenda kwenye Bwawa wa Umeme la Mwalimu Nyerere bwawa ambalo serikali imewekeza fedha nyingi kwa hiyo ni lazima kuendelea kulinda na kulinda vyanzo vya maji.”
Bashungwa alisema kutokana na kazi kubwa inayofanyika katika mradi huo mpaka sasa hakuna namna ambayo Serikali ya awamu ya sita itarejesha mradi huo kwa mtu yeyote.
“Kwa hiyo wale wote wanaodhani watatumia mbinu zozote kuwa shamba hili litarudi kwenye mikono ya watu hilo haliwezekani kwasababu tayari tumeshaona faida kubwa sana ya mashamba haya kuwa chini ya JKT.”
“ Na kama kuna watu wanataka ku-robby mashamba yarudi kwa watu sidhani kama jambo hilo lina nafasi katika serikali ya awamu ya sita kwa hiyo makamanda endeleeni kuchapa kazi tunajua tunalo deni la kuhakikisha vijana wanapata ajira na hapa tumeshuhudia mamia ya wananchi wa vijiji wamepata ajira na haya ndio maoni ya Mheshimiwa Rais wetu.”
“Mimi ni mhakikishie kwa imani aliyoionesha kwangu kumsaidia katika dhamana ya kumsaidia katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa itaendea kushirikiana na makamanda kuhakikisha maono yake na maelekezo yake hatumuangushi.”
Bashungwa alisema baada ya mafanikio walioanza kupatikana katika mradi huo, Wizara itahakikisha itaendelea kutenga fedha zaidi kwa JKT kuendelea kasi ya uzalishaji wa mbegu, kuweza kupata mahitaji ya chakula kwa vikosi kwa ajili ya vijana.
Kwa upande wa Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajab Mabele alisema mkati wa Jeshi ni kushiriki katika uzalishaji wa mbegu za nafaka ili kuhakikisha inachangia upatikanaji wa mbegu kwa wakulima
Naye Mkuu wa Wilaya Kilombero, Dunstan Kyobya alisema aliishukuru JKT kutekeleza mradi huo ambapo umechangia wananchi wake kupata ajira, kutumia kiwanda kuchakata mazao yao na ulinzi na kuahidi kuendelea ushirikiano.

Habari Zifananazo

Back to top button