Bashungwa: Miti barabarani ihudumiwe

DODOMA: WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewaagiza Wakala wa Barabara (TANROADS) kuendelea kupanda na kuhudumia miti iliyopandwa katika maeneo ya barabara kwa ajili ya kuendelea kupendezesha miji na kutunza mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Bashungwa amezungumza hayo katika Ofisi za Wizara zilizopo katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma leo Januari 29, 2024 wakati akiongoza zoezi la upandaji miti kwa ajili ya kuendeleza kampeni ya upandaji miti iliyozinduliwa na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango.

Ameitaka TANROADS kuhakikisha inaendelea kuhudumia miti walioipanda katika barabara ya Chimwaga – St.

Peter Claver (km 10), jijini Dodoma na kuwasisitiza kurudishia miti iliyokufa ili kuendelea kuboresha na kupendezesha eneo hilo.

“Hakikisheni TANROADS mnaihudumia miti mliyoipanda katika barabara ya Chimwaga – St.

Peter Claver (km 10), mnaiangalia kwa ukaribu na kupanda miti mipya kwa ile iliyokufa kama mlivyoelekezwa na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango,” amesema Bashungwa.

Bashungwa ametoa wito kwa watanzania kuendelea na tabia ya kupanda miti, wasisubiri kupewa maagizo kutoka kwa viongozi wakuu wa Serikali.

“Tabia ya kupanda miti iwe ni ya hiyari, tusisubiri hadi viongozi wakuu kusisitiza kufanya hivyo muendelee na tabia hii hata majumbani kwenu, ikiwa mti utakufa basi rudishieni mti mwingine tena.” Amesema Bashungwa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Mhandisi Aisha Amour, amesema kuwa zoezi hilo limeshirikisha upandaji wa miti tofauti zaidi ya 100 ikiwemo miti ya matunda na kivuli.

Balozi Aisha ameahidi kuendelea kuitunza miti hiyo na kuongeza miti mingine zaidi ili kuendelea kuifanya ofisi hiyo kuwa ya kijani.

Habari Zifananazo

Back to top button