Bashungwa: Veta, JKT kubalianeni
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa ameshauri kuwepo na makubaliano ya mafunzo ya ufundi baina ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Jeshi la Kujenga Taifa ( JKT).
Mafunzo ambayo yatafundishwa kwa vijana wanaopata mafunzo ya jeshi ili watakapomaliza wawe na mafunzo ya ujuzi.
Bashungwa ametoa ushauri huo alipotembelea banda la VETA katika maonesho ya nane nane kwenye viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya.
Bashungwa amesema iwapo VETA itaingia makubaliano hayo, vijana wanapomalinza mafunzo ya jeshi wanakuwa tayari na ujuzi unaotambulika.
Pia Bashungwa ameshauri vijana watakaopata mafunzo hayo kupewa cheti na VETA kitakachomtambulisha.
Akihitimisha ziara hiyo amewataka Wataalam ndani ya serikali na wakulima waendelee kujipanga na kutumia sherehe hizo kama jukwaa sahihi na la kimkakati la kuendelea kuonyesha bidhaa zao kwenye dunia.
Kwa upande wake Meneja Uhusiano wa VETA, Sittia Peter amesema mamlaka hiyo imeona kuna manufaa makubwa kama wataingia makubaliano hayo.
“Kwamba vijana watajifunza ukakamavu na miezi mingine mafunzo ya ufundi stadi ikiwa ni pamoja na kutunukiwa vyeti,” amesema.
Amesema vijana wanapopata mafunzo ya ufundi na kukosa cheti cha kuwatambua huwa wanakosa hata kupata fursa za kuendeleza ujuzi wao.