WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa amewasili mjini Istanbul, Uturuki na ujumbe wake kwa ziara ya kikazi, kufuatia mwaliko wa Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Yasar Guler kwa ajili ya kuhudhuria Maonesho ya Kimataifa ya viwanda vya Kijeshi.
Akiwa nchini humo, Bashungwa amepata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, kabla ya kutembelea Maonesho hayo ya Kimataifa ya viwanda Kijeshi.
Mazungumzo baina ya Mawaziri hao wa Ulinzi, yanalenga kuendeleza na kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya Wizara za Mataifa haya mawili kupitia sekta ya Ulinzi kwa ustawi wa Majeshi yetu pamoja na nchi hizi kwa ujumla.
Historia ya ushirikiano baina ya Tanzania na Uturuki ilianza tangu mwaka 1979, baada ya Uturuki kufungua Ofisi za Ubalozi wake jijini Dar es Salaam.
Ushirikiano baina ya mataifa haya mawili ni kupitia nyanja mbalimbali zikiwemo za uchumi, ulinzi, elimu, afya, utalii, mawasiliano pamoja na ziara za viongozi wa Kiserikali na Kijeshi wa Mataifa haya mawili kutembeleana.
Comments are closed.