WATU watano akiwemo mtoto mwenye umri unaokadiriwa kuwa miaka nane hadi tisa wamethibitika kufariki dunia, kadhaa wakijeruhiwa baada ya basi la New Force kugonga daraja na kuingia mtaroni katika kijiji cha Igando Kata ya Luduga Wilaya ya Wanging’ombe mkoani wa Njombe leo.
Taarifa zinaeleza kuwa dereva wa basi hilo lenye namba za usajili T173 DZU lililokuwa linatokea Dar es Salaam kwenda Rukwa alishindwa kulimudu wakati akilipita lori kabla ya kupoteza uelekeo.
Akizungumza kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, John Makuri Imori amesema taarifa zaidi zitatolewa baadaye.
“Kwa taarifa za awali basi la New Force lilikuwa linatoka Dar es salaam kwenda Rukwa, lilipofika Igando kuna sehemu ya daraja ‘likaovartake’ likapoteza uelekeo likagonga daraja likaingia mtaroni.
Tupo eneo la tukio kwa sasa hatujajua majeruhi ni wangapi lakini zenye uhakika hapa ni maiti tano wakiwemo wanaume wanne na mtoto mmoja”