Basi lisilotoa tiketi mtandao faini 250,000/-

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) imesema kuanzia leo mabasi yote ya abiria ambayo hayatakuwa yamewapa abiria wake tiketi za kielektroniki, hayataruhusiwa kuendelea na safari.

Imesema watakaokiri kosa watatozwa faini Sh 250, 000.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Latra, Salum Pazzy alisema jana watahakikisha mabasi yote yanatoa tiketi kidijiti.

Advertisement

Pazzy alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua matumizi ya tiketi mtandao kwa mabasi ya abiria yanayoenda mikoani na nchi jirani katika Kituo cha Mabasi cha Msamvu mkoani Morogoro.

Ukaguzi huo unafanywa na Latra kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani.

Ukaguzi huo wa tiketi mtandao ulifanywa kwa mabasi ya abiria 78 yaliyoingia na kutoka katika kituo hicho na ilibainika asilimia 98 ya wasafirishaji wanatumia tiketi hizo.

Pazzy alisema katika ukaguzi wao wamebaini mabasi yanayoenda nchi jirani hayajaanza kutoa tiketi mtandao na hivyo akawataka wamiliki wa vyombo hivyo vya usafiri watekeleze agizo hilo.

Alisema msafirishaji atakayebainika kutoa tiketi za mkono na akikiri kosa atatozwa faini ya 250,000 na ambao hawatakiri watashitakiwa mahakamani ambako faini yake ni Sh 500,000 au kifungo jela miezi sita au vyote viwili kwa pamoja.

Aliagiza abiria wote wapewe tiketi mtandao kuanzia mwanzo wa safari na hata wanaopandia njiani.

“Hivi kweli mtu anapandia gari Chalinze unashindwaje kumkatia tiketi mtandao kwa kisingizio cha kusumbuliwa na mtandao…hicho kitu hakikubaliki maana karibu eneo kubwa lina miji na mtandao upo wa kutosha,” alisema Pazzy.

Alisema walishawaongezea muda mara kadhaa na unatosha hivyo ni wajibu wa wasafirishaji abiria kutii sheria bila shuruti.

Abiria aliyekuwa kituoni hapo, Salama Ramadhani aliishukuru serikali na akasema awali walikuwa wanapata changamoto kwa kuwa gari likipata hitilafu walikuwa wanakosa msaada kutoka kwa wasafirishaji.