‘ Batuli Actress’ na wengine kuonekana Netflix

DAR ES SALAAM : MAFUNDI nguli watano wa Bongo Movie wamepanga kuanza kuuza kazi zao kupitia kampuni ya Netflix ya Marekani ili kufikia soko la dunia, na kuongeza thamani ya kazi zao.

Akizungumza na HabariLEO, mwigizaji Yobnesh Yusuph ‘Batuli’ ametaja wasanii wengine katika mpango huo kuwa ni Jacob Steven ‘JB’ Single Mtambalike ‘Richie’ Salim Ahmed ‘Gabo’ na Halima Yahya ‘Davina’.

Batuli amemwambia mwandishi wa mtandao wetu kuwa licha ya kuwa na mpango huo, ila pia wana mpango mwingine mwaka huu wa kufungua tovuti ya kuuza kazi zao.

Advertisement

“Ukiwa nchi yoyote duniani utaweza kulipia na kuangalia kazi zetu moja kwa moja kupitia website hiyo sisi watano tumeamua kufanya jambo la pamoja na utofauti,” amesema Batuli.

Wakati wakiwa katika mpango huo, Batuli ameiomba serikali kuandaa mfumo rafiki wa kuuza kazi zao kwani wadukuzi wamekuwa wengi kiasi ambacho baadhi ya wanaokamatwa hukumu zao zinakuwa nyepesi na hawalipi fidia.

Pia ameiomba serikali kuweka sheria kali ambayo itadhibiti wauzaji wa nakala feki, sambamba na hilo pia kuendelea kusaka soko la nje.

Batuli amezungumzia changamoto ya waigizaji wa Tanzania kushindwa kupenya nje ya Afrika ambapo amesema baadhi yao ni waoga na hawana uthubutu.

“Siamini katika lugha maana kuna nchi haziongei kingereza lakini waigizaji wao wapo kimataifa ninachoweza kusema kwa hili tunapaswa kujilaumu wenyewe makosa ya kutokujaribu,” ameongeza Batuli.

Batuli ambaye pia ni mfanyabiashara amesema anaamini kama angekuwepo marehemu Steven Kanumba basi angekuwa msanii wa kwanza kusainiwa na kampuni kubwa za kimataifa.

Mikakati yake na uthubutu nilikuwa navishuhudia, nadhani pia Idris Sultan, Wema Sepetu na Welu Sengo wamefanya kazi nchi za Afrika ingawa sijui kama kampuni kubwa,” ameeleza Batuli.