Bei mpya nyumba za Magomeni Kota zatangazwa

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA), umesema Rais Samia Suluhu Hassan ameongeza muda wa ununuzi wa nyumba 644 za Magomeni Kota kutoka miaka 15 hadi 30.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa TBA, Daud Kondoro amesema gharama za nyumba hizo kwa chumba kimoja ni Sh 48,522,913 na nyumba ya vyumba viwili inauzwa Sh 56,893,455.

Amesema baada ya Rais Samia kuzindua nyumba za Magomeni Kota Machi 23, 2022, alitoa maelekezo kuuzwa kwa nyumba hizo kwa wakazi hao kama Wakazi wanunuzi bila kuzingatia gharama za thamani ya ardhi, maeneo jumuishi kama ngazi, lifti na mandhari ya nje.

“Baada ya timu ya wataalam kufanya tathmini kwa kuzingatia maelekezo ya Rais, muda wa awali uliopangwa ni miaka 15 ikijumuisha miaka mitano ya kukaa bure,” amesema Kondoro.

Ameeleza kuwa baada ya mapendekezo hayo wakazi hao waliomba kuongezewa muda wa ununuzi wa nyumba hizo pamoja na kupunguziwa gharama hivyo, Rais Samia ameridhia kuwaongezea muda kutoka miaka 15 iliyoelekezwa na serikali awali hadi kuwa miaka 30 ikijumuisha miaka mitano ya kukaa bure.

“TBA tuko tayari kuwatambua wakazi waliotayari kutekeleza utaratibu huu wa
ulipaji na kuingia nao mkataba wa mkaazi mnunuzi na pia tuko tayari kuwatambua wakazi wasiokuwa tayari kutekeleza utaratibu huu licha ya kwamba wataruhusiwa kukaa bure kwa miaka mitano na baada ya muda huo kukamilika, watarejesha nyumba kwetu,” amesema.

Kondoro ameeleza kuwa wakazi hao watapaswa kutoa taarifa ya kusudio la kununua nyumba au kutonunua ndani ya siku 14 ili waweze kujibu.

Pia amesema ununuzi wa nyumba hizo utakuwa wa awamu ambapo katika mkataba huo, mkazi atapaswa kueleza ni utaratibu upi watautumia kulipia nyumba hizo na kwamba wenye uwezo wa kulipa kwa mkupuo wanaruhusiwa.

 

Habari Zifananazo

Back to top button