SIMIYU: Serikali imetangaza rasmi bei elekezi ya ununuzi wa zao la pamba katika msimu wa mwaka 2024/2025 kuwa ni Sh 1,150 kwa kilo moja ya pamba daraja la kwanza na daraja la pili ikiwa ni Sh 575 kwa kilo moja.
Bei hiyo imeongezeka kwa Sh 90 kutoka bei iliyotangazwa msimu wa mwaka jana 2023, ambapo kilo moja ilitangazwa kununuliwa kwa Sh 1,060.
Bei hiyo imetangazwa jana katika kijiji cha Ndoleleji wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga, ambao mbali na kutangazwa kwa bei ulizinduliwa rasmi msimu wa ununuzi wa zao hilo.
Isome pia https://habarileo.co.tz/wakulima-wa-pamba-macho-yote-shinyanga/
Akitangaza bei hiyo, Kaimu Katibu tawala mkoa huo Dafroza Ndalichako amesema kuwa wanunuzi wote wa pamba watatakiwa kununua kwa bei elekezi iliyotangazwa na serikali katika msimu huu.
Ndalichako amesema kuwa katika msimu huu wa ununuzi wa pamba, mfumo ambao utatumika kununulia zao hilo kwa wanunuzi wote ni mfumo wa ushirika, ambapo wakulima wote watatakiwa kuuzia pamba yao kwenye vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS).
“Kila mnunuzi wa pamba anatakiwa kwenda kwenye AMCOS kununua pamba, niwaagize pia viongozi wa Amcos kwenye mikoa yote inayozalisha pamba, kuhakikisha pamba inatunzwa vizuri bila ya kuwekwa uchafu wowote,” amesema Dafroza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Marco Mtunga aliwataka wakulima wa zao hilo kuzingatia ubora wa pamba kwa kuepuka kuweka maji, mchanga na kuhakikisha wanavuna katika utaratibu mzuri.
“Moja ya jambo ambalo linaweza kusababisha pamba yetu kushuka dhamani katika soko la kimataifa ni kuweka uchafu kama mchanga na maji, niwaombe wakulima kuzingatia usafi wakati wa kuvuta, tusichafue pamba,” amesema Mtunga.
Hata hivyo wakulima walionekana kutokukubaliana kwa bei iliyotangazwa, wakieleza kuwa bei hiyo ni ndogo na haiwezi kukidhi mahitaji yao kwani wametumia gharama kubwa katika kilimo.
“Kwa hii bei ambayo imetangazwa na serikali sisi wakulima hatukubaliani nayo, bei ni ndogo sana, hatukutarajia kabisa kutangaziwa bei hii, maana tumefanya kazi kwa kipindi kirefu sana lakini haiwezi kukidhi mahitaji yetu, tunamuomba Rais Samia atuongezee bei kidogo,” alisema Eliasi Sibani.