Bei ya petroli, dizeli yashuka

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei ya kikomo cha bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini ambapo bei ya petroli imeshuka katika baadhi ya mikoa.

Bei hizi zitaanza kutumika kuanzia leo saa 6:01 usiku. Taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo na kusainiwa na Mkurugenzi wa Ewura, Dk James Mwainyekule jana ilisema bei za rejareja za mafuta ya petroli na dizeli yaliyopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimeshuka kwa Sh 137 kwa lita na Sh 118/lita, mtawalia ikilinganishwa na bei za toleo la Juni 7 mwaka huu.

Pia, bei ya rejareja ya mafuta ya taa kwa Julai mwaka huu, itaendelea kuwa ni ile iliyotangazwa katika toleo la Juni 7, mwaka huu kwa kuwa hakuna shehena iliyopokelewa mwezi Juni mwaka huu.

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara), bei ya rejareja ya mafuta ya petroli imeshuka kwa Sh 188 kwa lita wakati bei ya mafuta ya dizeli imeongezeka kwa Sh 58 kwa lita ikilinganishwa na bei za toleo la Juni 7, mwaka huu.

Kwa mikoa ya Kusini (Lindi, Mtwara na Ruvuma), hakuna shehena ya bidhaa za mafuta iliyopokelewa kupitia Bandari ya Mtwara kwa Juni mwaka huu, hivyo bei ya rejareja ya dizeli kwa mwezi Julai itaendelea kuwa ni ile iliyotangazwa katika toleo la Juni 7.

Kutokana na upungufu wa bidhaa ya petroli katika maghala ya kuhifadhi mafuta yaliyopo Mtwara, waendeshaji wa vituo vya mafuta katika mikoa ya Kusini wanashauriwa kuchukua mafuta hayo kutoka katika Bandari ya Dar es Salaam.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa bei za rejareja za mafuta ya petroli katika mikoa hiyo zitazingatia bei kikomo ya rejareja ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji mpaka mikoa husika.

Aidha, kwa kuwa hakuna mafuta ya taa katika maghala yaliyopo katika Bandari za Tanga na Mtwara, waendeshaji wa vituo vya mafuta katika mikoa ya Kaskazini na Kusini wanashauriwa kuchukua mafuta hayo kutoka katika Bandari ya Dar es Salaam, hivyo bei za rejareja za mafuta ya taa katika mikoa hiyo zitazingatia bei kikomo ya rejareja ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji mpaka mikoa husika.

Taarifa hiyo ilibainisha kwamba tofauti ya bei kutoka sehemu moja kwenda nyingine inatokana na tofauti ya bei ya mafuta katika bandari ambayo mafuta yamepakuliwa na gharama za usafirishaji.

Pia mabadiliko hayo ya bei yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia, gharama za uagizaji na thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Marekani.

Hata hivyo, taarifa hiyo ilisema kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ili mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo au kushuka chini ya bei iliyoruhusiwa kama ilivyokokotolewa kwa mujibu wa Kanuni za Ewura za Kupanga Bei za Mafuta za Mwaka 2022 zilizotangazwa kupitia Gazeti la Serikali Na. 57 la Januari 28, 2022 na marekebisho ya Kanuni hii kama yalivyotangazwa kupitia Gazeti la Serikali Na. 421 la tarehe 23 Juni 2023. Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika zitokanazo na mauzo ya mafuta ya petroli.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x