Bei za petroli, dizeli zapungua

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza kupungua bei za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kuanzia leo.

Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Mwainyekule imeeleza kuwa bei za rejareja za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa yaliyopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimepungua kwa shilingi 187 kwa lita, shilingi 284 kwa lita na shilingi 169 kwa lita mtawalia, ikilinganishwa na toleo la Machi Mosi mwaka huu.

Dk Mwinyekule alieleza kuwa  kwa mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara), bei za rejareja za mwezi huu kwa mafuta ya petroli na dizeli zimepungua kwa shilingi 158 kwa lita na shilingi 231 kwa lita mtawalia ikilinganishwa na toleo la Machi Mosi mwaka huu.

Alieleza kuwa kwa mikoa ya Kusini (Mtwara, Lindi na Ruvuma) bei za rejareja za Aprili 2023 kwa mafuta ya petroli na dizeli zimepungua kwa shilingi 220 kwa lita na shilingi 176 kwa lita mtawalia ikilinganishwa na toleo la Machi Mosi mwaka huu.

“Mabadiliko haya ya bei yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia, gharama za usafirishaji na thamani ya shilingi ikilinganisha na dola ya Marekani,” alieleza Dk Mwainyekule.

Alieleza kuwa kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo au kushuka chini ya bei iliyoruhusiwa.

Taarifa ya Dk Mwainyekule ilieleza kuwa Dar es Salaam bei ya rejareja ya lita ya petroli Sh 2,781, dizeli Sh 2,847 na mafuta ya taa Sh 2,929.

Arusha petroli itauzwa Sh 2,813, dizeli Sh 2,957 na mafuta ya taa yatauzwa Sh 3,013. Dodoma lita ya petroli itauzwa Sh 2,840, dizeli Sh 2,905 na mafuta ya taa Sh 2,988.

Habari Zifananazo

Back to top button