Benjamin Mkapa kuongeza wigo tiba nguvu za kiume

MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Kanda ya Benjamin Mkapa, Dk Alphonce Chandika amesema wanajipanga kuongeza wigo wa kutoa huduma ya kupandikiza vipandikizi kwenye uume.

Dk Chandika alisema Dodoma jana kuwa wanafanya hivyo kutokana na mafanikio baada ya kupandikiza vipandikizi kwenye uume kwa wanaume wawili waliokuwa na changamoto ya nguvu za kiume.

Alisema hayo alipozungumzia utekelezaji wa majukumu na mwelekeo kwa mwaka 2023/24 katika utoaji wa huduma za afya kwa ubingwa bobezi.

Dk Chandika alisema Juni mwaka huu hospitali hiyo ilifanya upasuaji wa upandikizaji vipandikizi kwenye uume kwa watu wawili waliokuwa na matatizo ya nguvu za kiume na watu hao wamepona.

“Habari njema kutoka kwao mambo ni mazuri sana, tuliwapa masharti wakae wiki sita ndio wajaribu mitambo, mitambo inafanya kazi vizuri, tunaendelea kuwafuatilia wamesema matokeo ni mazuri na wamefurahi sana kwa sababu imerejesha heshima kwenye familia zao,” alisema.

Aliongeza: “Tulianzisha hii huduma baada ya kubaini uwepo wa changamoto kubwa ya nguvu za kiume.

“Tumeona waganga wa kienyeji wanapita mitaani na dawa za kutibu tatizo la nguvu za kiume na sisi kama taasisi ya umma, tukaona kwa nini tusije na mkakati wa kuwasaidia wananchi wenye changamoto ya nguvu za kiume.”

Dk Chandika alisema wataongeza wigo wa huduma hiyo ili ipatikane kwa yeyote anayehitaji.

“Wenzetu wanaotengeneza hivi vipandikizi wamefungua ofisi Dar es Salaam na wanakamilisha taratibu za usajili ili vipatikane kwa urahisi,” alisema.

Dk Chandika alisema mahitaji ya huduma hiyo ni makubwa na wao peke yao hawawezi kukidhi mahitaji hivyo wapo tayari kushirikiana na hospitali zingine.

Kwa mujibu wa Dk Chandika, gharama za huduma hiyo ni wastani wa Sh milioni sita mpaka milioni 10.

Kuhusu vipaumbele vya mwaka 2023/24, Dk Chandika alisema hospitali imetengewa zaidi ya Sh bilioni 64.5 na kati ya hizo Sh bilioni 18.6 zimeelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Alisema miradi hiyo ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa jengo la saratani na kwamba kwa mwaka huu umetengewa Sh bilioni 4.

Dk Chandika alisema fedha hizo pia zitatumika kuboresha huduma ya upandikizaji figo kwa kuwa na kituo mahususi kwa ajili ya huduma hiyo kitakachokuwa na vyumba vya madaktari, vyumba vya upasuaji, chumba cha ICU, maabara, duka la dawa na wodi.

Alisema fedha hizo pia zitasaidia kuongeza vyumba vya upasuaji hivyo kufanya kuwa na vyumba 10 kutoka vyumba saba vilivyopo sasa.

Dk Chandika alisema pia wamepanga kuanza maandalizi ya michoro na gharama kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha huduma za moyo.

“Tunakoelekea lile eneo halitoshi, tumeomba serikali kuanzisha mradi wa kuwa na jengo la peke yake kwa ajili ya ugonjwa wa moyo tu linalojitegemea,” alisema.

Alisema pia fedha hizo zitatumika kujenga mabweni kwa ajili ya wanafunzi na kuwaendeleza watumishi kwa ajili ya kuongeza ujuzi kwa ajili ya utoaji huduma bobezi.

Habari Zifananazo

Back to top button