Benki kusaidia ujenzi chuo cha ubaharia

BENKI ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imekubali kusaidia ujenzi wa Chuo cha Ubaharia ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kwenda na elimu ya uchumi wa buluu kwa wananchi wake ikiwemo kundi la vijana kuweza kujiajiri.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Abdulgulam Hussein wakati akijibu swali la mwakilishi wa Kojani kupitia ACT-Wazalendo, Hassan Hamad Omar aliyetaka kujua lini serikali itaanzisha chuo hicho ili kwenda sambamba na mikakati ya serikali kuingia katika uchumi wa buluu.

Akifafanua zaidi, alisema Zanzibar imeingia katika uchumi wa buluu ambapo chuo kitashughulikia masuala ya ubaharia.

Alisema kwa sasa AfDB imekubali kusaidia ujenzi wa mradi huo kupitia mpango wa kuimarisha taaluma za vijana katika ajira kukidhi soko la mahitaji ya uchumi wa buluu.

Alisema mradi huo unatarajiwa kuanza kufanya kazi katika mwaka 2023-2024 ambao kwa kiasi kikubwa utasaidia na kutoa ajira katika sekta ya uchumi wa buluu.

”Naibu Spika napenda kuwajulisha wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba Benki ya Maendeleo ya Afrika imekubali kujenga chuo cha ubaharia kupitia mpango wa kuimarisha taaluma za vijana katika ajira kukidhi soko la mahitaji ya uchumi wa buluu,” alisema.

Akitoa taarifa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed Mussa alisema kwa upande wa kisiwa cha Pemba maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho ni mchanga mdogo katika tawi la chuo cha Benjamin Mkapa.

Alisema kwa upande wa Unguja, tawi la chuo hicho linatarajiwa kujengwa Nkrumah nje kidogo ya mji wa Unguja ambapo lipo eneo la kutosha.

”Ujenzi wa chuo hiki ni muhimu ambapo tunaamini utasaidia kuwawezesha vijana kuingia katika uchumi wa buluu kwa mafanikio makubwa,” alisema.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button