Benki ya Dunia yatoa mabilioni Dar

BENKI ya Dunia imetoa mkopo wa Dola za Marekani milioni 200 (Sh bilioni 466.387) kugharamia mradi wa Bonde la Msimbazi ili kuepuka mafuriko na kuliwezesha Jiji la Dar es Salaam kukabili ongezeko la watu.
Fedha hizo zimeidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi Watendaji wa benki hiyo Septemba 30, mwaka huu. Gharama za mradi wote ni Dola za Marekani milioni 260 sawa na Sh bilioni 606.429.
Dola milioni 60 zitatolewa na Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa la Hispania ambalo litatoa Dola milioni 30 na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi itatoa ruzuku ya Euro milioni 30.
Hayo yamebainishwa na benki hiyo kupitia taarifa yao kwa vyombo vya habari jana. Benki ya Dunia imeeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo utasaidia kunusuru watu zaidi ya 300,000 wanaokabiliwa na changamoto ya mafuriko ya Mto Msimbazi zikiwamo jamii nyingi za kipato cha chini.
Kupitia fedha hizo, eneo ambalo hukumbwa na mafuriko katikati ya jiji litabadilishwa kuwa la kijani, la biashara na makazi ambalo litanufaisha wakazi wa Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini, Preeti Arora alisema kipaumbele katika mfumo wa ubia kati ya benki hiyo na Tanzania unazingatia ukuaji wa miji katika kukuza uchumi na kuzalisha ajira.
“Licha ya jukumu lake muhimu kama injini ya ukuaji wa taifa, mazingira ya biashara ya Dar es Salaam kwa kiasi kikubwa yameathiriwa kutokana na kutopangiliwa katika ukuaji wake, ufinyu wa huduma za mijini, kuathirika kwa makazi na miundombinu muhimu kutokana na mabadiliko ya tabianchi, hivyo msaada huu utasaidia kubadilisha jiji kuwa jiji lenye ufanisi zaidi,” alisema Arora.
Pia alisema watumiaji wa mfumo wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) na wasafiri wengine watanufaika na mradi huo wa Bonde la Mto Msimbazi unaofadhiliwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Kimataifa (IDA) kwa kiasi hicho cha fedha kwa kuwa utapunguza adha ya usafiri kutokana na mafuriko wakati wa mvua. Kwa mujibu wa benki hiyo, Dar es Salaam ina wastani wa wakazi milioni sita, inachukua asilimia 40 ya wakazi wote wa mijini nchini na huchangia asilimia 17 ya Pato la Taifa.
Dar es Salaam inakadiriwa kukua kwa kiwango cha asilimia 5.6 kila mwaka, hivyo inakadiriwa litakuwa jiji kubwa na idadi ya watu zaidi ya milioni 10 ifikapo 2030.
“Takribani asilimia 70 ya maendeleo katika jiji hilo sio rasmi na hayaambatani na upanuzi wa huduma huku likiwa na mifumo ya miundombinu iliyoundwa kwa ajili ya kuhudumia jiji dogo,” ilieleza benki hiyo.
“Kwa kuzingatia jiografia tambarare ya Dar es Salaam na mtandao mdogo wa mifereji ya maji, takribani kila msimu wa mvua husababisha mafuriko na eneo la chini la Mto Msimbazi huathirika zaidi,” alisema Mtaalamu Mwandamizi wa Miji wa Benki ya Dunia, John Morton.
Aliongeza: “Mradi huu umeundwa kustahimili ukuaji wa haraka wa miji na athari zinazotarajiwa za mabadiliko ya tabianchi kwa kuzuia mafuriko ambayo yanapunguza athari za uhamaji, mali, afya, maisha na wmaendeleo ya kiuchumi.” Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Victor Seff aliieleza HabariLEO kuwa Mradi wa Uboreshaji Bonde la Mto Msimbazi unatarajia kuanza Desemba 31, mwaka huu.
Seff alisema mradi huo utahusisha ujenzi wa daraja jipya la Jangwani, kupanua, kuongeza kina na kuimarisha kingo za Mto Msimbazi. Alisema mradi huo upo katika hatua mbalimbali za maandalizi na kwamba usanifu wa Daraja la Jangwani umekamilika na maandalizi ya nyaraka muhimu za mambo ya kijamii na mazingira yamekamilika.
Seff alisema pia upembuzi yakinifu na usanifu wa miundombinu ya Mto Msimbazi vimekamilika. Alisema mkataba wa mkopo kwa ajili ya mradi huo umeelekeza utekelezwe ndani ya miaka sita tangu usainiwe Septemba 30, mwaka huu.
“Taratibu za kuwapata wakandarasi wa ujenzi zitaanza mwezi Novemba mwaka 2022 na kazi za ujenzi za mradi huu zinatarajiwa kuanza ndani ya mwaka wa fedha 2022/23,” alisema Seff.
“Tutakapokuwa tunaingia mkataba na wakandarasi ndio tutajua muda halisi wa kazi, lakini ujenzi wa daraja unaweza kutumia miaka mitatu na uboreshaji wa Mto Msimbazi pia utachukua miaka mitatu,” aliongeza.