Benki yatakiwa kurahisisha mikopo kwa wafugaji, wavuvi

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ameitaka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) irahisishe upatikanaji wa mikopo kwa wafugaji na wavuvi wadogo.

Ulega alisema hayo Jumanne Dodoma wakati akimkaribisha waziri wake, Mashimba Ndaki kuzungumza katika hafla ya kutia saini Randama ya Upelekaji wa Fedha (MoU) kiasi cha Sh bilioni 60 kwa wavuvi na wafugaji wadogo.

Ulega alisema fedha iliyoidhinishwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya wavuvi na wafugaji samaki wadogo itawafikia walengwa.

Advertisement

“Jamani, Rais Samia ni real game changer (mwenye kubadilisha maisha). Kakubali kutoa pesa nyingi kwa wavuvi wadogo na wafugaji samaki bila riba. Haijapata kutokea. Tutahakikisha tunasimamia pesa hizi zinaenda kwa walengwa na kuleta matokeo tarajiwa,” alisema Ulega.

Aliwaelekeza viongozi na wafanyakazi wa TADB na kusema: “Oneni mfano huu wa utayari wa Mheshimiwa Rais Samia. Nanyi mbadilike na kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wafugaji na wavuvi.”

Hati hiyo ya makubaliano ilitiwa saini na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Rashid Tamatama na Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege.

Akihutubia Bunge mwaka jana jijini Dodoma, Rais Samia alionesha kutoridhika na mchango unaotolewa na sekta za mifugo na uvuvi katika maendeleo ya uchumi.

Aliahidi kufanya jambo ikiwamo kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wafugaji na wavuvi wadogo ili kuiinua sekta hizo ili zitoe mchango stahiki katika ukuaji wa uchumi.

 

 

1 comments

Comments are closed.