Benki yazindua akaunti ya mfugaji

DAR ES SALAAM: Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua ‘Akaunti ya Mfugaji’ mahususi kwa ajili ya wadau wa sekta ya ufugaji nchini wakiwemo wafugaji, wanenepeshaji mifugo, wafanyabiashara wa mifugo, wasafirishaji wa mifugo mifugo na wadau mbalimbali wanaohudumia sekta hiyo muhimu kiuchumi.

Huduma hiyo ya kwanza kutambulishwa na benki ya biashara nchini maalumu kwa kundi hilo, pamoja na kuchochea kasi ya ukuaji wa sekta hiyo kupitia huduma za fedha zilizorahisishwa zaidi pia inalenga kuunga mkono jitihada za serikali katika kuandaa uchumi jumuishi kwa makundi yote ya uzalishaji kupitia huduma bora za kifedha.

Hafla ya utambulisho wa huduma hiyo kitaifa imefanyika leo kwenye soko la mnada wa mifugo la Pugu lililopo wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam, ikiongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo (DC), Edward Mpogolo sambamba na viongozi wengine waandamizi wa wilaya hiyo, wadau wa biashara ya mifugo wakiwemo viongozi na wafanyabiashara wa soko hilo. Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo na Wakubwa wa benki ya NBC Elibariki Masuke aliwaongoza maofisa wengine wa benki hiyo kwenye uzinduzi huo.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, DC Mpogolo pamoja na kuipongeza benki ya NBC kwa kubuni huduma hiyo muhimu, alisema ujio wa huduma hiyo ni ukombozi mkubwa kwa wadau wa sekta ya mifugo nchini kutokana na uwepo wa changamoto ya ukosefu wa huduma za kibenki zinazoendana na mahitaji maalum ya kundi hilo hali ambayo imekuwa ikisababisha wengi wao kuamua kutumia huduma za kifedha zisizo rasmi na hivyo kuhatarisha usalama wao na fedha zao.

“Kwa mfano katika mnada huu wa Pugu unahusisha mzunguko wa fedha wastani wa kiasi cha Tsh bilioni 1 kila siku huku wengi wa wafanyabiashara wakilazimika kutembea na fedha taslimu kitu ambacho ni hatarishi kwao binafsi na mitaji yao. Hivyo ujio wa huduma hii ya Akaunti ya Mfugaji iliyobuniwa kwa ajili yao utakuwa suluhisho la changamoto hii kwasababu huduma za kifedha ikiwemo miamala zitapatikana kwenye maeneo ya minada hii karibu yao kabisa,’’ alisema.

Hata hivyo Mpogolo aliiomba benki hiyo kupitia huduma hiyo kuhakikisha inawasaidia zaidi wafugaji kwa kuwekeza zaidi kwenye suala zima la utoaji wa elimu ya fedha, elimu kuhusu ufugaji wa kisasa na elimu ya masoko ili wafugaji wawaweze kunufaika zaidi na idadi kubwa ya mifugo waliyonayo kupitia ufugaji na uwekezaji wa kisasa kwenye sekta hiyo.

Awali akiizungumzia huduma hiyo, Masuke alisema inahusisha wafugaji mmoja mmoja na vikundi huku ikitoa faida mbalimbali kwa wafugaji hao ikiwemo mikopo mbalimbali kwa waufugaji na biashara wa sekta hiyo huku ikiwa haiusishi makato ya uendeshaji wa akaunti kila mwezi, kupata taarifa za akaunti bila makato, gharama nafuu za utoaji wa fedha, huduma za kibenki kwa njia ya simu (NBC Kiganjani) huku muhusika akinufaika na nyongeza ya asilimia 2 kwenye akiba yake kila mwezi.

“Kwa upande wa wafugaji wa vikundi au vyama pia hawatakiwi kuwa na hofu sababu watakuwa na uhuru wa kuweka na kutoa fedha zao wakati wowote na pia watapata kitabu cha hundi kwa gharama nafuu wachotakiwa ni kufungua akaunti bure kabisa kwenye matawi yeto kote nchini,’’. Alisema.

Akifafanua zaidi kuhusu huduma hiyo Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wadogo, Lariba na wakulima kutoka Benki ya NBC, Bw Raymond Urassa alisema inahusisha wafugaji wa mifugo ya aina zote wakiwemo ng’ombe na kuku na hatua hiyo ni mwendelezo wa jitihada za benki hiyo kuyafikia makundi yote ya uzalishaji kufuatia uzinduzi wa huduma kadhaa za mahususi kwa wakulima ikiwemo bima ya afya.

“Ni karibuni tu tumetoka kuzindua huduma ya Bima kwa wakulima nchini nzima sambamba na sasa ni wakati muafaka pia kuwageukia wafugaji nao waweze kunufaika na huduma hizi za NBC mahususi kwao ikiwemo huduma hiyo ya bima,’’ alisema.

Wakizungumzia huduma hiyo, Mkuu wa Mnada wa Pugu, Noel Byamungu na Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mifugo kwenye mnada huo, Iddy Maziku walisema imekuja wakati muafaka na itakuwa suluhisho kwa wafugaji, wafanyabiashara wa mifugo na wadau wengine sokoni hapo ambao kwasasa baadhi yao wanalazimika kutembea na kiasi kikubwa cha fedha taslimu kwenye mifuko kutokana na kutokuwepo kwa huduma za kifedha zinazoendana na mahitaji yao karibu na maeneo ya minada hiyo.

“Ujio wa huduma hii utatusaidia kwa kiasi kikubwa sisi wadau wa sekta hii ya mifugo. Inawezekana tayari tunahudumiwa na taasisi za nyingine za kifedha zikiwemo zile ambazo sio rasmi lakini ujio wa huduma hii mahususi kwa ajili yetu itakuwa ni suluhisho na kambilio kwetu. Tunaamini kupitia huduma hii sasa hatulazimika tena kutembea fedha taslimu ili kufanya malipo ya manunuzi ya mifugo na huduma nyingine. Uzuri zaidi huduma hizi sasa zitakuwa zinatufuata mahali tulipo na hivyo kutuhakikishia usalama wetu na fedha zetu…kwa hili tunawashukuru sana NBC,’’ alisema Maziku.

Habari Zifananazo

Back to top button