BIASHARA ya binadamu hapa nchini bado ipo kwa kuwa mabinti wanasafirishwa kwenda nje ya nchi, pia wanatoka mikoani na kwenda Dar es Salaam, kufichwa kwenye baadhi ya nyumba na kufanyishwa kazi ambazo si sahihi.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema hayo alipokuwa akifungua Kongamano la Kimataifa kuhusu utumwa na maisha baada ya utumwa katika historia ya Afrika liliandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
“Na kesi nyingi tulizonazo hapa ni kwamba mabinti wanachukuliwa huko mikoani, wanaletwa hapa na wanafungiwa mahali na mpaka wahakikishe kwamba wamelipa fedha za yule aliyewaleta, aliyewanunulia nguo, aliyewakodishia sehemu hiyo na kuwanunulia mafuta na vitu vyote ambavyo ni vya kujipodoa anafichwa huko ndani.
“Akishamaliza deni lake ndio anaruhusiwa kuanza kutafuta fedha ambayo itakuwa ni yake mwenyewe kwa njia ambazo kwa hakika ni kama zinaakisi kabisa maisha yaliyokuwepo wakati wa utumwa.
” amesema Chalamila.
Amesema biashara hiyo ipo kwa kuwa mabinti huchukuliwa kutoka Dar es Salaam na kuelekea sehemu nyingine pia nchi za Afrika na nje ya Afrika.
Amesema mkoa wa Dar es Salaam wameanza kampeni muhimu ya kuhakikisha suala hilo linakomeshwa.
Amesema imani yake ni kwamba katika kongamano hilo la siku mbili linaloendelea mkoani Dar es Salaam litajadili suala hilo kwa upana kwa kuwa masuala ya utafiti huwa ni silaha katika kutoa elimu.
“ Basi nasi tutatumia mijadala hii katika kuhakikisha kuwa tunazirithi mbinu za kitaaluma ambazo watakuwa wamejadili na kuona namna gani tunaweza kuzitumia sasa kuondokana na masuala ya biashara ya binadamu,”amesema.
Kwa maelezo ya Chalamila amesema utumwa kama mfumo wa maisha uliokuwepo unaweza kuwa ulibeba athari kubwa za kimaendeleo, kitamaduni, za kisiasa, na hata masuala ya kiuchumi.
Naye Mhadhiri Mwandamizi Idara ya Historia na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano hilo, Dk Salvatory Nyanto amesema kumekuwepo na changamoto nyingi na mijadala anuai kuhusu utumwa baada ya kukomeshwa nini kilitokea,
Baada ya sheria kupitishwa kukomesha utumwa hao watumwa walikwenda wapi, na kwa nini siku hizi kuna utumwa wa kisasa kwa hiyo masuala hayo ndio yaliyosababisha kuwepo kwa kongamano hilo la kimataifa.
Amesema njia mojawapo ya kukomeshwa kwa utumwa huo na aina mbalimbali za utumwa ni kuwepo kwa majadiliano na kuwepo kwa tafiti ili kutumia tafiti hizo kutunga sera na miongozo mbalimbali inayoweza kukomesha biashara hiyo pamoja na utumwa wa kisasa katika jamii mbalimbali za kiafrika.
“Sababu zinazochangia kuwepo kwa utumwa wa kisasa ni kutokuwepo kwa serikali madhubuti hasa katika maeneo ya Afrika ya Kati na Afrika Magharibi, machafuko mbalimbali yaliyokuwa yakitokea yamesababisha kuwepo kwa utumwa huo wa kisasa, watu wamekuwa wakipelekwa kwenye maeneo mbalimbali,” amesema.
Ametaja sababu nyingine ya utumwa wa kisasa ni kumekuwepo na matamanio ya kuisha maisha mazuri, “sasa watu wanapotamani kwenda sehemu Fulani au maisha mazuri wamekuwa wakijikuta wanaingizwa katika utumwa wa kisasa na utumwa huo wa kisasa umekuwa ukifanyika ukiratibiwa na mawakala ambao wanatumia njia mbalimbali kurubuni na kushawishi watu wakiamini wakivuka mipaka ya nchi yao wanakuwa na maisha mazuri na kwa bahati mbaya hali imekuwa sio hivyo,”.