Biashara ya kujiuza isifumbiwe macho

HAPO zamani ilikuwa ikifanywa na wachache na katika mikoa kama wa Geita kwa kificho. Lakini sasa mambo yamebadilika kipindi hiki cha utandawazi. Ni biashara inayoshamiri tena ikifanywa waziwazi.

Utafiti wangu mdogo unaonesha kwamba biashara hii iliyozoeleka pia kuwa ya ‘watu wa mjini’ sasa ipo hata vijijini, ikifanyika hata mbele ya makazi.

Zipo sababu mbalimbali zinatajwa kuchangia tatizo hili.

Wapo wanaosema ugumu wa maisha ndio chanzo, na wengine wakiamini ukosefu wa ajira ndio kiini cha kushamiri biashara hii. Binafsi nalitazama kama anguko kubwa la maadili na malezi kwenye jamii zetu. Ni anguko ambalo linazalisha kizazi kisicho na haiba kinachohalalisha biashara ya hovyo, biashara haramu.

Mbali na kwamba haijawahi kuwa utamaduni wetu wala shughuli halali, lakini sasa mambo yamekuwa ndivyo sivyo, inashangaza kuona biashara inafanyiwa mpaka matangazo. Mitandao ya kijamii imekuwa ndio jukwaa kuu la matangazo huku nyumba za kulala wageni zikigeuka kuwa ofisi rasmi za biashara hii inayofanywa na vijana kwa watu wazima.

Kinachosikitisha zaidi ni kuona wimbi kubwa la vijana wa jinsia zote, kwa maana ya vijana wa kiume na wa kike wote wamejitosa kuuza miili yao wakiamini ndio chanzo chao cha kipato. Kuna watu wanaweza kuwanyooshea kidole wasichana lakini hawawezi kujitosa kwenye biashara hii kama hakuna soko kwa hiyo wanaume wanaosababisha soko la wasichana wanaojiuza pia ni wa kunyooshewa kidole. Hali ilivyo kwa sasa si ya kukaa kimya.

Kuna ulazima wa kukaa chini, kutafakari na kuchukua hatua madhubuti kuweza kukabiliana na tatizo hili linaloendelea kutafuna kizazi cha leo. Hili ni suala mtambuka, ni suala ambalo linagusa jamii ya Watanzania wote bila kujali taasisi, dini na kabila na hivyo ipo haja ya kuunganisha nguvu kupiga vita tatizo hili linaloharibu kizazi na nguvu kazi.

Huu siyo muda wa kujiuliza tulipokosea, huu siyo muda wa kumtafuta mchawi, huu siyo muda wa kujutia bali ni muda wa kung’amua ukubwa wa tatizo na njia sahihi za kuliondoa. Viongozi wa dini, serikali na taasisi za umma na binafsi tusimame kidete, tueleze madhila na madhara ya tatizo kwa maslahi ya taifa ili kuokoa kizazi cha sasa na baadaye na kuendelea kujenga Tanzania yenye uadilifu.

Kama nilivyosema, hili si suala la umaskini kwa sababu kila mara zipo njia mbadala za kufanya mkono uende kinywani isipokuwa tatizo la maadili. Ni vyema, sheria zitungwe kupiga marufuku jambo hili badala ya sasa ambapo wasichana wanaojiuza maarufu kama machangudoa wanapokamatwa hupewa kesi za uzururaji.

Ni vyema hata wanaume wanaotoa soko (machangu papa) pia wakawa wanakamatwa ili kulinda maadili. Kwa pamoja tukemee biashara ya ngono, tuikatae na tuweke mipango thabiti ya kuzalisha kizazi chenye uimara wa kimwili, kiakili na kifikra ili kuimarisha nguvu kazi muhimu kwa maendeleo ya taifa. Jamii pia ihimize ndoa halali kwa wingi ili watu kuepuka matendo haya ya hovyo.

Habari Zifananazo

Back to top button