Biashara ya madini yazidi kupaisha mapato

KATIBU Mtendaji wa Tume ya Madini, Yahya Samamba amesema kuanzia kipindi cha Julai 2022 hadi Machi, mwaka huu, biashara ya madini imechangia Sh bilioni 471.7 sawa na asilimia 92.62 kupitia mrabaha na ada ya ukaguzi kwenye mapato ya serikali na kuifanya sekta ya madini kuendelea kufanya vizuri.

Samamba aliyasema hayo juzi jijini Dodoma kwenye kikao kazi cha Kamisheni ya Tume ya Madini chenye lengo la kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa majukumu ya tume kwa kipindi cha miezi mitatu.

Alieleza kuwa masoko ya madini 42 pamoja na vituo vya ununuzi wa madini vilivyoanzishwa nchini vimeongeka ambako vituo vya ununuzi wa madini 84 vilivyokuwepo hadi Desemba 2022, vimeongezeka hadi 93 kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Machi, mwaka huu na kuchangia Sh bilioni 117.6. Samamba alisema siri ya kufanya vizuri kwenye masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini nchini ni usimamizi mzuri unaofanywa na watumishi wa Tume ya Madini kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali.

Advertisement

Akielezea hali ya ukusanyaji wa maduhuli kwa ujumla, Samamba alifafanua kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai 2022 hadi Machi, mwaka huu, tume ilikusanya jumla ya Sh bilioni 509.3 sawa na asilimia 83.61 ya lengo la makusanyo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 ambalo ni Sh bilioni 822.

Aliongeza kuwa tume bado inaendelea kuweka mikakati ya ukusanyaji wa maduhuli ili kuhakikisha lengo lililowekwa na serikali linavukwa ifikapo Juni mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Samamba alisema tume imeendelea kutatua changamoto mbalimbali kwenye shughuli za utafiti, uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini kupitia ziara mbalimbali zinazofanywa na viongozi waandamizi wa tume, sambamba na kuendelea kutoa elimu kuhusu afya, usalama na utunzaji wa mazingira kwenye migodi ya madini.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *