Biashara ya mbaazi Tanzania, India mambo safi
NEW DELHI, India: TANZANIA imeruhusiwa kuiuzia India kiasi cha mbaazi inachoweza kuanzia sasa hadi Machi 2025.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo Februari 24, 2024 wakati wa mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki January Makamba, na Mwenyeji wake Waziri wa Biashara na Viwanda wa nchini humo Piyush Goyal yaliyofanyika jijini New Delhi.
Kadhalika, katika mazungumzo hayo viongozi hao wamekubaliana Tume ya Pamoja ya Biashara kukutana mwezi Aprili 2024, ili kuweka mikakati ya pamoja ya kukuza biashara baina ya Tanzania na India.
Awali kabla ya kufikiwa kwa makubaliano haya, Tanzania iliruhusiwa kuuza kiasi cha tani laki mbili za mbaazi nchini India kwa mwaka.
Waziri Makamba alikuwa nchini India kushiriki mkutano huo sambamba na kufuatilia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini humo mwezi Oktoba 2023.