Biashara ya nguo yadorora kuelekea sikukuu
ZIKIWA zimebaki siku nne kuadhimishwa kwa sikukuu ya Krismasi, wafanyabiashara wa nguo mkoani Dar es Salaam wamesema biashara ya bidhaa hizo kwa msimu wa mwaka huu imedorora ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
HabariLEO lilifanya mahojiano na wafanyabiashara katika maduka mbalimbali mkoani humo ili kujua uhalisia wa mauzo katika msimu huu wa kuelekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Imebainika kuwa hali ya mauzo hususani katika tarehe hizi za ukingoni, hayaridhishi ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Mfanyabiashara wa nguo za kiume katika eneo la Buguruni, John Kimambo alisema tangu Desemba 12 hadi jana, aliuza suruali mbili na fulana mbili za watoto wa familia moja ambao waliambatana na baba yao dukani hapo.
“Miaka yote nafanya biashara lakini mwaka huu ni mgumu kibiashara sijapata kuona, hata kufungasha mzigo mkubwa wa matoleo mapya nimeshindwa nikihofia hasara maana zilizopo pia ni fasheni mpya lakini utokaji wake wa kusuasua,” alisema.
Kwa upande wa eneo la Kariakoo, wafanyabiashara pia walisema wateja si wengi ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Mfanyabiashara wa Mtaa wa Congo, Salum Kondo, alisema, “tunamshukuru Mungu kuuza kiasi fulani lakini huwezi kulinganisha na wakati kama huu mwaka jana. Unaweza kuona kundi kubwa la wateja dukani wanauliza bei, unamuuliza una shilingi ngapi ndiyo kwanza umemfukuza.”
Baadhi ya mafundi vyerehani pia walikiri kutokuwapo mrundikano wa vitambaa vinavyosubiri kushona kama ambavyo ilizoeleka katika msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
Fundi cherehani na mkazi wa Yombo Vituka, Zuberi Mbwana alisema nguo wanazoshona ni za wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza na za sikukuu ni chache.