JESHI la Polisi mkoani Morogoro, linamshikilia Nestory Elias (62), mkazi wa Bon’gola, Kata ya Kilakala, Manispaa ya Morogoro kwa tuhuma za mauaji ya Mwajuma Sadru (75), mkazi wa mtaa wa Bong’ola.
Bibi huyo anadaiwa kuuawa na mwili wake kutelekezwa, kisha kufunikwa kwa mawe umbali wa mita 180, kutoka nyumbani kwake eneo la Kwa Maskini.
Kamanda wa Polisi Mkoa Morogoro, Fortunatus Musilimu amesema leo kuwa tukio hilo la mauaji lilitokea leo Oktoba 3, 2022 saa 12 asubuhi mtaa wa Bong’ola.
Musilimu alisema inadaiwa marehemu alipigwa na kitu kizito kichwani na kwamba polisi walifika eneo la tukio na kuchukua mwili kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Alisema uchunguzi wa awali unaonesha marehemu alikuwa na mgogoro wa ardhi na mtuhumiwa huyo, ambaye katika kipindi kisichojukikana aliachiwa kwa msamaha wa Rais kutumikia kifungo jela.
Hata hivyo hakuweka wazi kuwa mtuhumiwa huyo alifungwa miaka saba bila kutaja makosa yake na mwaka ambao alipata msamaha wa Rais na kwamba uchuguzi bado unaendelea.
Wakizugumzia tukio hilo, mtoto wa marehemu John Dofriana, alisema kuwa alipata taarifa za kutoonekana kwa mama yao, akiwa jijini Dar es Salaam hatua iliyomfanya kusafiri hadi mkoani Morogoro na kuanza kumtafuta ndipo walikuta mwili wake ukiwa umetelekezwa ukiwa umefunikwa na mawe.
Alisema kuwa mama yake alikuwa akiishi kwa miaka mingi katika mtaa huo na alikuwa akiishi na dada wa kazi, huku akihudumiwa kwa karibu na mwanaye mkubwa hadi tukio hilo la kikatili lilipomkuta.
“Kimsingi tukio limetokea jana (Oktoba 2,2022) usiku na kaka aliporudi nyumbani kutoka kwenye majukumu yake alikuta tukio limeshatokea na alijaribu kupigia simu, lakini ilikuwa haipokelewi na wakati akiendelea kumtafuta ndipo waliipata simu ikiwa na damu nyingi ndipo wakagundua mama ana shida na mimi nikaanza safari usiku huo kuja Morogoro,” alisema John.
Naye jirani na nyumba ya marehemu, Tatu Juma, alisema kuwa bibi huyo anayefahamika kwa jina la mtaani kama Bibi Mzungu, alikuwa mcheshi na alikuwa na uhusiano mzuri na watu.