Bidhaa za Tanzania kuingia Uingereza bila tozo

TANZANIA ni moja kati ya nchi zinazoendelea itakayonufaika na Mpango wa Biashara wa nchi Zinazoendelea wa Uingereza (DCTC) unaotarajiwa kuanza mapema mwakani.

Kwa mujibu wa Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar mpango huo ukianza asilimia 99 ya bidhaa za Tanzania zinazoingia Uingereza zitaingia nchini humo bila kulipiwa ushuru. Balozi huyo alisema mpango huo pia utahusisha bidhaa zinazozalishwa nchini zikitumia vifaa kutoka nchi nyingine.

Kwa mujibu wa ubalozi huo, mpango huo utakaoanza mapema mwakani, utasaidia kukuza biashara, kuibua ajira na kukuza uchumi katika nchi hizo zinazoendelea ikiwemo Tanzania. Aidha, ripoti inayoelezea mpango huo inabainisha kuwa mpango huo mpya unazipa nchi zinazoendelea upendeleo wa kibiashara katika nchi yoyote duniani.

Aidha, unaonyesha dhamira ya Uingereza ya kujenga uhusiano wa muda mrefu, wenye manufaa kwa pande zote na nchi zinazoibukia kiuchumi ambazo ni nyumbani kwa zaidi ya watu bilioni 3.3. Ripoti hiyo inaeleza kuwa DCTC ni hatua kuu katika kukuza biashara huria na ya haki na mataifa yanayoendelea na utatumika kwa nchi zinazoendelea 65, ukitoa ushuru wa chini na mahitaji ya sheria ya kusafirisha hadi Uingereza.

Ilieleza kuwa mpango huo husaidia nchi kubadilisha bidhaa zao nje na kukuza uchumi wao, huku kaya na biashara za Uingereza zikinufaika kutokana na bei ya chini na chaguo kuwa kubwa zaidi.

Mpango huo ulitengenezwa kwa msaada wa wananchi ambapo watu 300 kutoka sekta binafsi, wafanyabiashara na nchi zinazoendelea walishiriki na kutoa mapendekezo. Mashauriano hayo yalionyesha azimio la Uingereza la kuboresha ufikiaji wa soko kwa nchi zinazoendelea.

Habari Zifananazo

Back to top button