Biharamulo mbioni kupata maji ya uhakika

WIZARA ya Maji  imetenga zaidi ya Sh  milioni 850 kwa ajili ya ujenzi wa chanzo cha maji kutoka Ziwa Victoria, ili kuunganisha maji katika mji mdogo wa Biharamulo na kuimarisha huduma ya maji katika mji huo.

Waziri wa Maji Juma Aweso amesema kuwa hivi karibuni wakazi wa Biharamulo wataanza kupata huduma ya maji ya uhakika kupitia Mamlaka ya Maji ya Biharamulo, baada ya mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kuanza kutekelezwa na kusimamiwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Bukoba Mjini (BUWASA).

Advertisement

Alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo  umetokana na ziara ya Rais  Samia Suluhu Hassan aliyoifanya mkoani Kagera  na kupitia Wilaya ya Biharamulo, ambapo wananchi  na Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Ezra Chiwelesa, waliomba  huduma ya maji na  suluhu ya kudumu juu ya upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo.

“Tayari serikali imesikia kilio chenu , nakumbuka  Mheshimiwa Rais alipopita hapa mlisema vyanzo vimekauka, maji ni machafu, tunapata maji muda mchache, naamini upatikanaji wa maji kutoka Ziwa Victoria utakuwa ndilo jibu lenu la kupata maji saa 24, “amesema  Aweso.

Waziri huyo katika ziara yake alizindua tanki la maji lenye ujazo wa lita milioni moja, ambalo limeimarisha huduma ya maji katika mji  wa Biharamulo, ambalo limegharimu zaidi ya Sh Milioni 300.

Kwa mujibu wa  Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Mji wa Biharamulo, Siraji Basiga  kukamilika kwa tanki hilo kumeanza kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa saa 12.

7 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *