SERIKALI imetenga Sh bilioni 10 kwa ajili ya mikopo nafuu kwa ajili ya waendeshaji vituo vidogo vya kusambaza bidhaa ya petroli vijijini.
Kupitia Wakala ya Nishati Vijijini (REA), serikali imekuwa ikihamasisha na kuwezesha miradi ya kusambaza nishati ya umeme vijijini ukiwemo wa kuhamasisha ujenzi wa vituo hivyo vidogo vya kusambaza bidhaa za petroli vijijini kwa njia ya mikopo nafuu.
Vilevile imetenga Sh trilioni 6.7 kwa ajili ya kufikisha miundombinu ya umeme katika vitongoji 36,101 vilivyobaki katika jumla ya vitongoji 64,760.
Akizungumza jijini hapa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Hassan Said alisema ili kuhakikisha mradi huo wa vituo vya petroli vijijini unafanikiwa katika mwaka 2023/2024, serikali imetenga Sh bilioni 10 kwa ajili ya mikopo nafuu kwa waendelezaji.
Katika kutekeleza mradi huo, mwananchi anayetaka kuwekeza atapewa mkopo kuanzia Sh milioni 50 hadi 75 kwa riba ya asilimia tano na atarejesha katika kipindi cha miaka saba na sasa REA inaendelea kupokea maombi ya waombaji na mwisho wa kupokea maombi ni Agosti 25, mwaka huu.
Saidi alisema Rea pia inasambaza umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili ambao unahusisha kupeleka umeme kwenye vijiji 4,071 kati ya vijiji 12,318 na unakusudia kuunganisha wateja wa awali 258,660.
Mradi huo unafadhiliwa na serikali pamoja na Benki ya Dunia (WB) kwa sasa upo katika hatua ya utekelezaji na umefikia asilimia 73 na utakamilika Desemba 2023 kwa mikataba 32 na utakamilika Juni 2024 kwa mikataba saba.
Umeme kwenye vitongoji Said alisema baada ya serikali kukamilisha kupeleka umeme katika vijiji, imepanga kupeleka umeme kwenye vitongoji na tayari utambuzi umefanyika na kubaini kwamba vitongoji 36,101 tu havijafikiwa na umeme kati ya vitongoji 64,760 vilivyopo Tanzania Bara.
Serikali ilipata mkopo Sh bilioni 100 wa gharama nafuu kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) fedha ambazo zitatumika kuanza kutekeleza mradi huo kufikisha umeme katika vitongoji 654 katika mikoa ya Songwe na Kigoma na hivyo kufanya vitongoji vilivyobaki nchini kuwa 36,101.
Mradi wa nishati safi Rea pia inatekeleza mradi wa nishati safi ya kupikia vijijini ambapo kupitia mradi wa usambazaji mitungi ya gesi ya kupikia (LPG) inakusudia kusambaza mitungi ya gesi 71,000 yenye thamani ya Sh bilioni tatu pamoja na majiko banifu 200,000 katika maeneo ya vijijini.