KATIKA mwaka 2015 hadi 2020, serikali kupitia mapato ndani ya halmashauri nchini imetoa Sh bilioni 133 kwa ajili ya vikundi vya vijana, wanawake na wenye ulemavu.
Katika kipindi hicho, jumla ya Sh bilioni 92.21 sawa na asilimia 69.32 zilirejeshwa kutoka kwenye vikundi vya wanufaika.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni Dodoma Jumatano na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi, Dk Festo Dugange wakati akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni, Tarimba Abbas (CCM).
Tarimba alitaka kujua kiasi kilichokopeshwa kwa vikundi vya wanufaika mwaka 2015 hadi 2020.
“Katika mwaka 2015-2020, serikali kupitia mikopo ya ndani ya halmashauri imetoa shilingi bilioni 133. Katika kipindi hicho jumla ya shilingi bilioni 92.21 sawa na asilimia 69.32 zimerejeshwa kutoka vikundi vya wanufaika,” alisema.
Katika swali la nyongeza mbunge Tarimba alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni, Hanifa Suleiman Hamza katika kipindi cha mwaka jana ambao alitoa fedha za mikopo kwa asilimia 100 ambazo ni Sh bilioni 3.5 kwa watu wa Kinondoni.
Kisha akahoji, “kwa kuwa mikopo iliyotolewa kwa vikundi haikuwa asilimia 100 na ni asilimia 31 fedha hazijarejeshwa, serikali haioni vema kufanya ukaguzi ili kujua mikopo hiyo inawafikia walengwa na kwa nini haijarejeshwi?”
Dk Dugange alisema ni kweli kwamba katika kipindi cha miaka mitano marejesho hayakuwa asilimia 100.
“Hata hivyo, serikali ilifanya ukaguzi maalumu kwa halmashauri zote 184 na kuweka mkakati wa kuhakikisha mikopo hiyo inarudishwa.”
Serikali iliziagiza halmashauri zote kuweka katika orodha na kubainisha vikundi vyote ambavyo vilikopeshwa na vinarejesha fedha hizo.
Alisema serikali imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa kutoa mikopo na urejeshaji mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kutoka kwa vikundi vya vijana, wanawake na wenye ulemavu.
Mfumo huo wa kielektroniki unasaidia kujua kiwango cha mikopo na urejeshaji wake kwenye halmashauri zote 184 nchini.