SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema imetenga Sh bilioni 2.3 kwa ajili ya mradi wa ofisi ya Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi (ZIPA) inayotarajiwa kujengwa Mazizini Mjini Unguja.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Kamati ya Uchumi ya Baraza la Wawakilishi kuhusu ripoti ya mamlaka hiyo kutoka kwa wajumbe.
Soraga alisema upo umuhimu wa kuwepo kwa jengo la kisasa la Ofisi ya Uwekezaji Vitega Uchumi (Zipa) ambayo itakuwa na hadhi ya kisasa ya kuendesha shughuli za uwekezaji.
Alisema shughuli za uwekezaji zimeimarika kutokana na serikali kufungua milango ya uwekezaji, ambapo ni muhimu kuwepo kwa ofisi itakayokuwa na hadhi ya kushughulikia na kuendesha mambo ya uwekezaji.
“Serikali imesikia kilio cha wajumbe wa kamati ya uchumi kuhusu ukosefu wa ofisi ya kisasa ya Mamlaka ya vitega uchumi itakayoendesha shughuli za kusimamia wawekezaji….tumetenga shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Zipa,” alisema.
Mapema Soraga alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane ilipoingia madarakani ilifanya juhudi kubwa za marekebisho ya Zipa kukifanya kuwa kituo kimoja cha uwekezaji katika shughuli zote kwa wawekezaji.
Alisema hatua hizo kwa kiasi kikubwa zilirahisisha malengo na madhumuni ya wawekezaji kuwekeza kwa kupata vibali vya uwekezaji katika kipindi kifupi.
“Mamlaka ya Uwekezaji na Vitega Uchumi sasa ni kituo bora cha uwekezaji katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki kwa kuwavutia wawekezaji kuwekeza,” alisema.
Akifafanua zaidi alisema urasimu uliokuwepo awali wa wawekezaji kuhangaishwa na kuchukua muda mrefu kufuatilia katika taasisi na wizara mbalimbali kupata vibali, sasa haupo.
Alisema hatua ya kuifanya Mamlaka ya vitega uchumi kuwa kituo kimoja kwa kiasi kikubwa ni fursa nyingine adhimu ya kuwavutia wawekezaji kuwekeza.
”Kuwepo kwa kituo kimoja cha uwekezaji maana yake sasa tumefanikiwa kuondoa urasimu uliokuwa ukiwakabili wawekezaji kuwekeza Zanzibar,” alisema.