Bil 3.8/- kujenga kivuko Mwanza
SERIKALI kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) imesaini mkataba wa ujenzi wa kivuko kitakachogharimu Sh bilioni 3.8.
Temesa imeeleza kivuko hicho kitatoa huduma katika maeneo ya Buyagu na Mbalika Wilaya za Sengerema na Misungwi mkoani Mwanza.
Mkataba kati ya serikali na kampuni ya Songoro Marine ya Mwanza umesainiwa katika viwanja vya Sabasaba wilayani Sengerema.
Kivuko hicho kitakapokamilika kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kubeba tani 50 zikijumuisha; abiria 100 (waliokaa 50 na waliosimama 50) na magari madogo sita.
Katika hafla hiyo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya alisema ujenzi wa kivuko hicho ni juhudi ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha huduma kwa jamii.
‘’Ujenzi wa kivuko hiki utakapokamilika utaharakisha shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa wananchi waishio katika Wilaya ya Sengerema, Misungwi na maeneo mengine, aidha inatarajiwa kuwa na usafiri wa uhakika wenye huduma bora na salama katika maeneo ya Buyagu na Mbalika.’’ Alisema Kasekenya.
Aliwaagiza Temesa wausimamie mradi huo ili kivuko hicho kijengwe kwa ufanisi, kwa wakati na pia thamani ya fedha zinazotumika izingatiwe.
Kasekenya alisema madhumuni ya ujenzi wa kivuko hicho ni kuwapatia wananchi usafiri salama na wenye uhakika kwa kuwa wamekuwa wakitumia mitumbwi kwenye eneo hilo lenye takribani kilometa saba.
Mtendaji Mkuu wa Temesa, Lazaro Kilahala alisema ujenzi wa kivuko hicho kitaondoa kero za kiuchumi na kijamii ambazo zimekuwa zikichelewesha maendeleo ya wananchi.
Kilahala amesema Ujenzi wa vivuko vipya na ukarabati wa vivuko na miundombinu yake ni muendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025.
‘’Katika mwaka huu wa fedha, wakala unaendelea na ujenzi wa vivuko vipya vitano vyenye thamani jumla ya shilingi bilioni 33.2 vitakavyotoa huduma kwenye vituo vya Kisorya – Rugezi, Bwiro – Bukondo, Nyakarilo – Kome, Ijinga – Kahangala na Mafia – Nyamisati hivyo kivuko cha Buyagu-Mbalika ambacho leo mkataba wake wa Ujenzi umesainiwa ni kivuko cha sita (6) ambacho Ujenzi wake unaanza katika mwaka huu wa fedha,‘’ alisema.
Kilahala aqlisema sambamba na ujenzi wa vivuko vipya pia Temesa inakarabati vivuko 18 na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vivuko katika maeneo 11 ya huduma kwa gharama ya shilingi bilioni 27.5.
Mbunge wa Misungwi, Alexander Mnyeti amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan Samia Suluhu Hassan kwa kazi anazoendelea kuzifanya kwenye majimbo ya Kanda ya Ziwa.
Mbunge wa Sengerema, Hamis Tabasam alisema wananchi wa Wilaya ya Sengerema wanaishukuru serikali kwa miradi inayotekelezwa katika wilaya yao.