Bil 44/- kuboresha afya, elimu Ilemela

MANISPAA ya Ilemela mkoani Mwanza imetumia Sh bilioni 44 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya afya na elimu.

Kutekelezwa kwa miradi hiyo kumekidhi Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26) inayoelekeza miradi hiyo ikamilike kwa wakati.

Mkurugenzi Mtendaji wa manispaa hiyo, Modest Apolinary alitaja miradi iliyotekelezwa kwa upande wa sekta ya afya kwa fedha za ruzuku kutoka serikali kuu kuwa ni ujenzi wa kituo cha afya Kayenze uliogharimu Sh milioni 500, ukamilishaji wa zahanati tatu mpya katika mitaa ya Lumala, Nyamadoke na Masemele na Sh milioni 150 zimetumika kwenye utekelezaji wake.

Apolinary alitaja miradi mingine ni ujenzi wa jengo la upasuaji, wodi mbili, jengo la kuhifadhi maiti na kuchomea taka katika hospitali ya wilaya katika eneo la Kabusungu kwa gharama ya Sh milioni 800 na miradi yote hiyo imekamilika kwa asilimia 100.

Alitaja miradi mingine ni ujenzi wa wodi ya wazazi katika kituo cha afya Buzuruga uliotengewa bajeti ya Sh milioni 203 na hadi sasa umetumia Sh milioni 50.

Apolinary alisema mradi mwingine ni ukamilishaji wa jengo la kujifungulia katika zahanati ya Ilemela uliotengewa Sh 906,712,800, ukamilishaji wa jengo la kujifungulia katika zahanati ya Nyakato uliogharimu Sh milioni 40.

Kwenye sekta ya elimu, Apolinary alitaja miradi iliyotekelezwa ni ujenzi wa madarasa 97 katika shule za sekondari kwa fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19. Umegharimu Sh bilioni 1.94, ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Buzuruga iliyotengewa Sh milioni 600.

Apolinary alitaja miradi mingine ni kukamilisha vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, ofisi za walimu, vyumba na matengenezo ya madawati katika shule za msingi na sekondari kwa fedha za mapato ya ndani.

Alisema manispaa hiyo pia imejenga kituo cha mabasi na maegesho ya malori cha Nyamhongolo kwa gharama ya Sh bilioni 26.6.

Alisema mradi wa kuwezesha kuchochea shughuli za maendeleo katika Jimbo la Ilemela uliogharimu Sh milioni 60.3  ikiwa ni fedha kutoka serikali kuu na umetekelezwa kwa asilimia 100.

Apolinary alitaja mradi mwingine ni wa ufyatuaji wa matofali kwa ajili ya ujenzi wa maboma kwa fedha za mapato ya ndani uliotengewa Sh milioni 250 na hadi sasa Sh 226,947,500.

Mradi mwingine wa kiuchumi ni kuwezesha ukarabati wa masoko kwa ajili ya kuboresha mazingira kwa wafanyabiashara wadogo kwa fedha za mapato ya ndani, ambapo walitenga Sh milioni 175 na kiasi cha Sh 71,556,085 zimetumika ikiwa ni sawa na asilimia 41.

Aliongeza kuwa halmashauri inatarajia kuchangia Sh bilioni 1.2 katika bajeti ijayo ya mwaka wa fedha 2022/23.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button