Bil 5/- kukopesha wamachinga

MKURUGENZI wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru amesema Sh bilioni tano zitatolewa kwa ajili ya mikopo na miongoni mwa wanufaika wa mikopo hiyo ni wafanyabiashara ndogondogo walio katika maeneo rasmi.

Alisema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari juzi akizungumzia kukamilika kwa soko la Machinga Complex na mikakati ya jiji kuwaimarisha wafanyabiashara kiuchumi.

Mafuru alisema katika mwaka huu wa fedha, Sh bilioni tano zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.

Advertisement

“Kila robo ilikuwa ikitoka shilingi bilioni moja sawa sawa na shilingi bilioni nne kwa mwaka, lakini mwaka huu tutatoa shilingi bilioni tano,” alisema.

Alisema hiyo ni fursa pia kwa wafanyabiashara kujiunga kwenye vikundi ili wakopesheke hasa wale walio katika maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya kufanyia biashara ikiwamo Soko la Machinga Complex lililopo eneo la Bahi Road.

Pia alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya kazi zao kwenye maeneo yanayoruhusiwa.

“Tumefanya usanifu wa maeneo mapya, tumetenga shilingi milioni 700 kwa ajili ya eneo la kufanyia biashara lililopo kati ya Stendi Kuu na Soko la Job Ndugai ili kuwezesha watu wa maeneo ya barabara kuu ya Dar es Salaam kufaidika na fursa,” alisema.

Alisema eneo la mnada mpya pia kutakuwa na eneo maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara.

“Wafanyabiashara ndogondogo wote watakuwa kwenye maeneo rasmi ya kufanyia biashara, lengo ni kuweka jiji katika mpango mzuri na liwe safi,” alisema.

Aidha, alisema Dodoma City Hotel itaanza kazi Novemba Mosi mwaka huu na sasa taratibu za ununuzi zinaendelea.

Pia hoteli ya Jiji ya Mtumba Investment yenye nyota tano itaanza kazi Novemba Mosi mwaka huu na ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100.

 

 

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *