KAMATI ya Kudumu ya Bunge inayosimamia masuala ya Ukimwi, Kifua Kikuu, Dawa za Kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza imeagiza watendaji wa halmashauri wasimamie fedha zinazotolewa na wahisani na serikali kwa ajili ya utekelezaji mradi wa Timiza Malengo.
Mradi huo unatekelezwa kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2021 hadi 2023 katika halmashauri 18 za wilaya kwenye mikoa ya Dodoma, Geita, Morogoro, Singida na Tanga ukilenga vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 24.
Kwa mujibu wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020, chama hicho kinatambua kuwa virusi vya Ukimwi (VVU) na upungufu wa kinga mwilini (Ukimwi) una madhara kwa jamii na maendeleo ya Taifa kwa ujumla na mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi ni endelevu na yanahitaji juhudi za pamoja.
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/2022 kuhusu mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi umeainisha shughuli zilizotekelezwa ukiwemo ununuzi na usambazaji wa dawa za kufubaza makali ya VVU katika ngazi za utoaji wa huduma za afya nchini na waathirika milioni 1.3 wamepatiwa dawa za kufubaza makali ya VVU.
Mpango huo umeainisha kutolewa kwa ruzuku kwa watoto 15,983 walioko kwenye programu ya majaribio ya kuwawezesha wasichana balehe na wanawake vijana (AGYW) kubaki shuleni na kuwa salama dhidi ya maambukizi mapya ya VVU.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene alisema mradi wa Timiza Malengo unagharimu Sh bilioni 55 kwa ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Ukimwi, Kifua kikuu na malaria (Global Fund) wasichana balehe na wanawake vijana wapatao 1,000,000 watafikiwa na mradi huo.
Simbachawene alisema hayo Juni mwaka huu Dodoma wakati wa uzinduzi wa ugawaji vishikwambi kwa walimu wa shule za msingi na sekondari.
Alisema lengo la mradi huo ni kusaidia vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 24 kutimiza ndoto zao na kuwasaidia vijana walio ndani na nje ya shule kwa kuwajengea uwezo wa fikra, maarifa na maadili ili wawe salama dhidi ya maambukizi ya VVU.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayosimamia masuala ya Ukimwi, kifua kikuu, dawa za kulevya na magonjwa yasiyoambukiza, Dk Alice Kaijage alisema fedha za utekelezaji wa mradi huo zinatolewa na serikali ya Marekani kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania.
Dk Kaijage akizungumza mjini Ifakara wilayani Kilombero mkoani Morogoro wakati wa ziara ya kawaida ya Kamati hiyo kutembelea kuona afua zinazotekelezwa na serikali ikiwemo ya kupambana na Ukimwi.
“Kama tutakuwa tunazisimamia vizuri fedha hizo utakuta watu wanakuwa na mabadiliko makubwa ya kimaisha na ile tofauti ya kimaisha cha kutoka mtu aliyenacho na asiye nacho kitaendelea kubadilika siku hadi siku,” alisema Dk Kaijage.
Kamati iliagiza watendaji wa halmashauri wahakikishe fedha zinapotolewa zinawafikia wahitaji ili waepuke vishawishi.
Alisema kwa Mji wa Ifakara vijana wameonesha ujasiri kwa kufungua miradi, kujiendeleza kielimu na kujihusisha na biashara ukiwemo ufugaji kuku, nguruwe na vibanda vya kuuza bidhaa za vyakula.
“Tumeona vijana wamekuwa na uwezo wa kuanzisha miradi, kukodi mashamba, kutengeneza nyumba kwenye familia zao, kununua viwanja na fedha hii kwa kweli imesaidia kiasi kikubwa sana na kamati imeridhishwa na kazi iliyofanyika,” alisema Dk Kaijage.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Kaspar Mmuya alisema afua za Ukimwi hazitekelezwi na wizara moja na kuna wadau wa ndani ya nchi na nje ya nchi yakiwemo Shirika la Vijana Nchini (TAYOA) na Shirika la Afya na Utafiti Afrika (AMREF).
Mmuya alisema serikali katika kupambana na Ukimwi imejielekeza ifikapo mwaka 2030 kusiwe na maambukizi mapya ya VVU na kusiwe na yeyote mwenye VVU ambaye atakufa kwa Ukimwi sanjari na kuondoa unyanyapaa kabisa ifikapo mwaka huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dk Leonard Maboko alisema mradi wa Timiza Malengo ni kwa ajili ya wasichana balehe na wanawake vijana hasa walio katika mazingira magumu.
Dk Maboko alisema kuanzishwa kwa mradi huo kulitokana na kiwango cha maambukizi ya Ukimwi wakati huo kila mwaka yanapotokea maambukizi mapya asilimia 40 ya maambukizi hayo yalikuwa yanatokea kwa vijana waliokuwa na umri wa miaka 15 hadi 24.
Alisema mradi huo umeweza kuwafikia wasichana balehe na wanawake vijana kwa huduma jumuishi ya kinga dhidi ya maambukizi mapya ya VVU na elimu ya ujasiriamali.
Dk Maboko alisema wasichana wengi wameweza kujitambua na kusimama imara katika biashara ikiwa ni pamoja na kuanzisha vikundi kwa ajili ya kurahisisha kufikiwa na huduma.
Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Jacob Kayange katika taarifa ya mkoa huo kwa kamati hiyo alisema Sh 1,178,195,000 zilipokelewa kwa ajili ya ruzuku ya ujasiriamali kwa wasichana 1,966 kutoka halmashauri tano za mkoa huo waliopata mafunzo na Sh milioni 742.7 zimelipwa kwa walengwa.
Kayange alisema mradi pia ulitoa mafunzo ya mama vijana 114 yaliyohusu mafunzo bora ya makuzi na matunzo ili waweze kuwafundisha wasichana namna ya kuwalea watoto vizuri kwa kuzingatia utaratibu wa makuzi ya mtoto.
Alisema wasichana 8,289 walipatiwa elimu bora ya makuzi na malezi ya watoto.