Bil 580/- zaenda kaya maskini
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) imetumia zaidi ya Sh bilioni 580.2 kuwalipa walengwa kutoka kaya maskini tangu kuanza kipindi cha pili cha Mpango wa Kuziwezesha Kaya Maskini ulioanza mwaka 2020.
Pia kaya mpya zaidi ya 200,000 zinatarajiwa kuingizwa katika mpango huo baada ya kukamilika taratibu za kuwapata.
Haya yalibainishwa jijini hapa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), Ladislaus Mwamanga alipozungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki.
Alisema Sh 580,297,395,975 zimetumika katika miaka mwili na nusu hadi sasa ya utekelezaji wa kipindi cha pili cha mpango huo.
Mpango wa kwanza wa kunusuru kaya maskini ulioanza mwaka 2012, hadi kufika mwaka 2019 ulikuwa na kaya za walengwa 1,118,752 ambazo zilitambuliwa kutoka asilimia 70 ya vijiji, mitaa na shehia zote nchini.
Kipindi cha pili cha awamu ya tatu kilichoanza Februari 2022 umeweza kuongeza kaya lengwa hadi kufikia 1,371,038 zenye watu zaidi ya milioni 5 ambao ni asilimia 55 ya kaya zinazoishi katika mazingira magumu hapa nchini.
Aidha, Mwamanga alisema baada ya kukamilika kwa mchakato wa kuzitambua kaya maskini, zaidi ya kaya 200,000 zinatarajia kuingizwa katika mpango huo.
Hatua hiyo inafuatiwa na hatua ya kuondoa kwenye mpango takribani kaya 173,076 baada ya kuhitimu ifikapo Januari 2023.
Kaya hizo ni pamoja na 56,586 zinazoondolewa kutokana na kuimarika kiuchumi na kuweza kujitegemea bila ruzuku na kaya ya walengwa 16,490 ambazo zinapokea ruzuku ya uzalishaji.
“Katika mpango wetu tuna kaya zaidi ya 200,000 ambazo zinatarajia kuingia katika mpango wetu, ndio maana tumefanya tathimini walioimarika ili watoke wapishe na wengine waweze kuingia,” alisema.
Alisema hatua ya kufanya mchakato wa kaya zilizoachwa ni katika kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan aliyeagiza kuwarudia ambao wameachwa na mpango kwa sababu moja au nyingine.
“Awamu ya kwanza tulifikia asilimia 70 ya vijiji, mitaa na shehia, awamu ya pili tukamalizia asilimia 30, lakini bado kuna wengine ambao wamesahaulika na Rais Samiaa aliagiza tuwarudie wote walioachwa ili nao waingine na tunatarajia kaya zaidi ya laki mbili zitaingia baada ya hawa kuondolewa na hili zoezi ni endelevu,” alisema.