Bil 6.4/- kuwajengea uwezo wahadhiri vyuo vikuu

SERIKALI ya Awamu ya Sita imetoa Sh bilioni 6.4 katika mwaka huu wa fedha kuwajengea uwezo wahadhiri na viongozi wa vyuo vikuu kuhusu utoaji elimu vyuoni.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Charles Kihampa wakati akielezea mafanikio ya miaka miwili ya taasisi hiyo chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wake na waandishi wa habari Dodoma jana.

Profesa Kihampa alisema TCU ina ushirikiano na taasisi mbalimbali za Afrika na duniani kwa ujumla, hivyo serikali inawawezesha kwenda kujadiliana na wenzao na kujifunza namna wanavyoendesha vyuo vyao.

Kutokana na hilo, alisema wameendelea kuandaa na kuratibu mafunzo kwa viongozi, wahadhiri na maofisa wa vyuo vikuu vya umma na binafsi kuwajengea uwezo katika usimamizi na uendeshaji wa taasisi zao.

“Kuanzia mwaka wa fedha 2022/23, Serikali ya Awamu ya Sita imetenga shilingi bilioni 6.4 kupitia mradi wa elimu ya juu wa mageuzi ya kiuchumi kwa ajili ya kuimarisha uthibiti ubora na uhuishaji wa mitaala ya vyuo vikuu ambavyo mitaala zaidi ya 300 ya vyuo vikuu iko katika hatua mbalimbali za kufanyiwa mapitio ili kuhuisha kwa kuzingatia maoni ya wadau ili kukidhi matarajio yao na mahitaji ya soko,” alisema Profesa Kihampa.

Kwa mujibu wa Profesa Kihampa, kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana, jumla ya viongozi na wanataaluma 575 walinufaika na mafunzo hayo ambayo yalilipiwa na serikali kupitia fedha hizo kwa asilimia 100.

Pia alisema viongozi wa vyuo vikuu 10 kutoka vyuo vya umma na binafsi watapata fursa ya kutembelea nchi nyingine katika vyuo vikuu vikubwa duniani ili kujifunza namna wenzao wanavyoendesha vyuo vyao.

Aliyataja mafanikio mengine ya TCU chini ya Serikali ya Awamu ya Sita kuwa ni kuimarika kwa mifumo ya uthibiti ubora, ushauri na usimamizi wa elimu inayotolewa na vyuo vikuu nchini ili kuhakikisha vyuo vikuu vinaendana na mwelekeo wa nchi ambapo Tanzania imelenga kuwa taifa la watu wenye maarifa, ujuzi, weledi na uwezo wa kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi zinazowakabili wananchi ifikapo mwaka 2025.

Katika kuhakiki ubora, alisema TCU imeimarisha mifumo yake ya ushauri na ukaguzi wa mara kwa mara kwa vyuo vikuu vyote 47 nchini.

“Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa fursa za masomo ya elimu ya juu na idadi ya wanafunzi wanaosoma katika vyuo vya elimu ya juu nchini; nafasi za masomo katika elimu ya juu kwa programu za shahada ya kwanza zimeongezeka kutoka 157,770 mwaka 2020/21 hadi 172,168 mwaka 2022/23, ongezeko hili ni la nafasi 14,398 sawa na asilimia 9.1,” alisema Profesa Kihampa.

Alisema programu za masomo zilizoruhusiwa kudahili wanafunzi wa shahada ya kwanza nazo zimeongezeka kutoka 686 mwaka 2020/21 hadi 757 mwaka 2022/23.

Pia wanaodahiliwa katika shahada ya kwanza nao wameongezeka kutoka 87,934 mwaka 2020/21 hadi kufikia 113,383 mwaka 2022/23.

Profesa Kihampa alisema katika miaka hiyo miwili ya uongozi wa Rais Samia, idadi ya wanafunzi wanaosoma vyuo vya elimu ya juu nayo imeongezeka kutoka 259,266 mwaka 2020/21 hadi kufikia 295,519 mwaka 2021/22.

Pia alisema TCU imeimarisha programu za elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu elimu ya chuo kikuu ili kuwafikia wadau wengi ikiwamo kutembelea wahitimu wa kidato cha sita waliopo katika mafunzo ya JKT ili kuwaelimisha kuhusu elimu ya chuo kikuu na udahili.

Pia kuandaa maonesho ya elimu ya juu, sayansi na teknolojia ambayo hufanyika kila mwaka Dar es Salaam.

Habari Zifananazo

Back to top button