SERIKALI imetumia zaidi ya Sh bilioni 65 kulipia matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) baada ya kuongeza umri wa wategemezi wa watumishi wa umma kutoka miaka 18 hadi 21.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama alisema hayo jijini Mwanza wakati akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
“Tumefanya kwa muda wa miaka miwili kwa watumishi 6,000 sasa, lakini pia lazima tuzungumze ili kila mtumishi aone nani mwenye sifa ya kufanyiwa categorization,” alisema Jenista.
Aliongeza: “Bado tunakwamishwa na baadhi ya watumishi wachache, kwa sababu tunapokea malalamiko mengi sana jinsi tulivyowakabidhi madaraka wale wanaosimamia rasilimali watu wanavyotoa haki.”
Alitoa mfano wa kukaimisha madaraka, kufanya teuzi za nafasi za madaraka kwenye ofisi za umma bado kuna upendeleo kwa kuwa watumishi wa umma wenye sifa huachwa kupewa ukaimu ama wanathibitishwa watu ambao hawana sifa.
Alisema serikali imeamua kutengeneza mwongozo ili kupanga na kutengeneza uwajibikaji wa pamoja kwa kuweka kiwango kitakachotumiwa na waajiri wote kutoa haki kwa watumishi wa umma.
Alisema serikali imekamilisha ujenzi wa mifumo miwili ya kupima utendaji kazi wa mtumishi wa umma na utendaji wa taasisi za serikali.
Alisema mfumo uliotumika awali wa Opras haukukidhi matakwa ya mwajiri katika kuona ukweli na uhalisia wa kazi za kila siku za mwenendo wa mtumishi wa umma.
“Kwa hiyo tumeshafanikiwa kujenga mfumo mmoja wenye moduli mbili; ya kwanza itapima utendaji kazi wa mtumishi kwa saa, siku, wiki, mwezi, robo mwaka na kwa mwaka,” alisema Jenista na kuongeza kuwa moduli nyingine itapima utendaji kazi wa taasisi za umma.
Alisema miaka ijayo serikali inafikiria kupima utendaji kazi kwa mtumishi wa umma kwa kutumia kipimo cha kisasa ili kubaini mtumishi anayekuwepo kazini ajulikane yupo na asiyekuwepo ajulikane pia.
“Tutakwenda taratibu, lakini tutafika mahali tunataka haki ya msingi kwa mtumishi iweze kupatikana kwa kutumia vigezo yaani key performance indicators (viashiria vya msingi vya utendaji), kwa kumzawadia mtumishi ama kumuadhibu,” alifafanua.
“Sasa tunatengeneza mfumo utakaotusaidia kukagua utendaji kazi wa kila siku wa kila taasisi hapa nchini ili tuweze kupunguza mienendo ya kutozingatia maadili kwa watumishi,” aliongeza Jenista.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima alisema alichokisema waziri ni ujumbe kwa watumishi wote wa umma kwa kuwa ametoa mwelekeo wa kitaifa.