SERIKALI imedhamiria kumaliza uhaba wa mbegu ili kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuwekeza kwenye uzalishaji wa mbegu bora.
Waziri wa Kilimo Hussen Bashe aliliambia HabariLEO hivi karibuni kuwa kutokana na malengo hayo, Rais Samia Suluhu Hassan aliamua kuongeza bajeti katika eneo la uzalishaji wa mbegu bora hadi kufika Sh bilioni 83 ili kumaliza uhaba wa mbegu.
Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2020 inaeleze kuwa chama kitahakikisha ndani ya miaka mitano taifa linaendelea kujitosheleza kwa chakula kwa kuwa na upatikanaji wa uhakika wa pembejeo na zana za kilimo.
Chama hicho kimesisitiza kuhusu matumizi ya mbegu bora za mazao na kuongeza kuwa juhudi za uzalishaji wa mbegu bora zimefanikiwa ambapo zimeongezeka kutoka tani 36,614 mwaka 2015 hadi kufikia tani 71,208 mwaka 2020.
CCM imesema kuwa ongezeko hilo ni sawa na asilimia 94.5 huku uzalishaji wa mbegu bora ndani ya nchi ukiongezeka kutoka tani 20,605 mwaka 2015 hadi kufikia tani 66,032 mwaka 2020.
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2021/22 – 2025/26 umeitaja Sekta ya Kilimo kuwa ndio kitovu cha ukuzaji wa viwanda na maisha ya watu nchini, ambapo inakadiriwa kuwa asilimia 58.1 ya watu wanapata kipato kutokana na shughuli za kilimo.
Kwa kipindi chote cha utekelezaji wa mpango, juhudi zitaelekezwa katika kuunganisha na kuimarisha mafanikio yaliyopatikana na kuzingatia fursa zinazopatikana kutokana na mbinu bora za kilimo zinazozingatia hali ya hewa pamoja na matumizi ya mbegu bora.
Bashe alisema hadi Aprili 2022, asilimia 26.68 ya mbegu bora zilikuwa zimepatikana sawa na tani 49,962.35 za mbegu bora huku mahitaji ya nchi yakiwa ni tani 187,197 kwa mwaka.
Alisema Kati ya mbegu hizo, tani 35,199.39 zimezalishwa ndani ya nchi, tani 11,340.2 zimeingizwa kutoka nje ya nchi na tani 3,422.80 ni kiasi kilichobaki katika msimu wa kilimo uliopita.
Taarifa ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo ya Mwaka 2022/23 ilisema Wizara kupitia Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) itaendelea kuthibiti ubora wa mbegu nchini kwa kukagua mashamba ya mbegu na kupima ubora wake kwenye maabara.
Kwa mujibu wa bajeti hiyo hadi Aprili, 2022 TOSCI ilikuwa imekagua hekta 1,654.2 za mashamba ya mbegu na kubaini yote yamekidhi vigezo vya ubora ambapo imekusanya sampuli 1,795 na kupima ubora wake ambapo sampuli 1,591 zilikidhi vigezo vya ubora, sampuli 143 hazikukidhi vigezo vya ubora na sampuli 61 zinaendelea kufanyiwa vipimo.
Taarifa ya bajeti hiyo ilisema mwaka 2021/2022, kamati ya Taifa ya Mbegu iliidhinisha aina 18 za mbegu kwa ajili ya matumizi zitakazochangia katika upatikanaji wa mbegu bora msimu wa 2022/2023.
“Kati ya mbegu hizo, aina tano zimegunduliwa na TARI na aina 13 zimegunduliwa na kampuni binafsi za mbegu ambazo zinatoka katika mahindi, choroko, ngano, tumbaku, mpunga na viazi mviringo,” alisema Bashe wakati akisoma bajeti hiyo.