Bil 90/- kunufaisha wakulima wa korosho

SERIKALI imetoa Sh bilioni 90 kwa ajili ya kutoa ruzuku ya viuatilifu kwa ajili ya wakulima wa korosho katika msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023.

Hayo yamebainishwa jijini hapa na Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Francis Alfred wakati wa kutoa taarifa ya utekelezaji shughuli za bodi kwa mwaka 2021/2022 na mwelekeo wa utekelezaji wa mwaka 2022/2023.

Alisema katika mpango wa serikali wa kutoa ruzuku kwenye pembejeo,  wakulima wa korosho wamepewa Sh bilioni 90 kwa ajili ya viuatilifu vya zao  hilo.

Advertisement

Alfred alisema mpaka sasa viuatilifu vilivyosambazwa msimu wa 2022/2023 ni sulphur ya unga tani 14,600, viuatilifu vya maji lita 2,600,000 na mabomba 1,216.

Alisema kwa msimu wa kilimo uliopita wa mwaka 2021/2022, serikali ilitoa ruzuku ya viuatilifu vyenye thamani ya Sh bilioni 59.356 vilivyotolewa kwa wakulima wa korosho bure.

Kuhusu ubanguaji korosho, Alfred alisema tani 30,000 za korosho zinatarajiwa kubanguliwa nchini kati ya tani 400,000 zinazotarajiwa kuzalishwa.

Alisema msimu uliopita jumla ya tani 8,959.023 za korosho ghafi zilibanguliwa ndani ya nchi kati ya tani 240,158.752 zilizozalishwa sawa na asilimia 3.7.

Bodi ya Korosho Tanzania inaendelea na maandalizi ya usimamizi wa masoko na mauzo ya korosho ghafi ili kuhakikisha msimu wa mwaka 2022/2023 unakuwa na mafanikio kwa wadau wa tasnia ya korosho nchini.