“Bila Kinana kusingekuwa na Bashungwa huyu mnaemjua”
KAGERA: WAZIRI wa Ujenzi ambae pia ni Mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa amesema asingefika hapo alipofika kama sio Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana.
Amesema, Kinana ameifanyia makubwa CCM na serikali na vijana wengi wanasiasa wamekua wakikimbilia kwake kusaka ushauri.
Bashungwa amemwaga sifa hizo katika sherehe za kuweka Wakfu Kanisa Kuu, Usharika wa Lukajange, Dayosisi ya Karagwe.
Amesema, mwaka 2016 alisumbuliwa sana na baadhi ya watu wa Karagwe lakini Kinana alimpa ushauri ambao anaufuata mpaka leo na umemuimarisha.
“Vijana wengi tunamkimbilia sana, nilipokua nasumbuliwa hapa aliniambia Bwana mdogo achana na hao watu kawatumikie wananchi, tatua kero zao, wananchi ndio wamekuweka hivyo usimpoteze muda kushughulika na wanaokusumbua.
“Nenda kwa wananchi, maana mwisho wa siku wao ndio watakuhoji tumekupa ubunge mbona hatukuoni?
” Utakapoanza kujitetea ohoo kulikua na migogoro watakuhoji, sisi tulikutuma ukagombane na fulani na fulani, umetufanyia nini ?
Ulikua wapi?…..: “Akanionya nisiingie katika hiyo changamoto.
” Namshukuru sana nitaendelea kufuata ushauri wake ili nisiwakwaze, kwa heshima hiyo nampa zawadi ya ng’ombe jike, ” amesema Bashungwa na kukabidhi Kinana kamba ya kufungia ng’ombe kama ishara.