SERIKALI imetenga Sh bilioni 2 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya ujenzi wa wodi za kulaza wagonjwa wa ndani na ujenzi wa uzio katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu.
Naibu Waziri wa Afya, DkGodwin Mollel ametoa taarifa hiyo leo bungeni jijini Dodoma alipojibu swali lililoulizwa na mbunge wa viti maalum, Ester Lukago Midimu aliyehoji lini Serikali itajenga uzio katika Hospitali ya Mkoa wa Simiyu?
Akijibu swali hilo kwa niaba ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Dk Mollel amesema Waziri Ummy alishaielekeza wizara kufanya tathimini ya madaktari bingwa na ubingwa bobezi kujua idadi yao katika maeneo waliopo ili kusambazwa nchini kulingana na mahitaji ya huduma za ubingwa bobezi katika mikoa.
Oktoba 7, 2023 hospitali hiyo ilipokea vifaa tiba mbalimbali kutoka Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Ziwa, kwa ajili ya kuanza kutoa huduma za kibingwa kwa akina mama wajawazito na watoto hivyo kuondoa changamoto ya wajawazito na watoto waliohitaji huduma hizo kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya kanda Bugando, mkoani Mwanza.